NEWS

AFYA

STORI ZA KITAA

Latest Release

Wednesday, 8 November 2017

Na Mathias Canal, Dodoma
Serikali imesema kuwa utekelezaji wa mpango wa Kilimo Kwanza umekuwa na mafanikio katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara nchini ambapo uzalishaji wa jumla wa mazao ya biashara katika msimu wa mwaka 2016/2017 umeongezeka kufikia Tani 881,583 ukilinganisha na Tani 796,562 katika msimu wa mwaka 2015/2016.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa amebainisha hayo Leo Novemba 7, 2017 Bungeni Mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi Mkoani Singida Mhe Yahaya Omary Masare aliyetaka kufahamu Kuna mafanikio kiasi gani kwa mazao ya biashara na chakula kwani Katika mpango wa kilimo Kwanza serikali ilihamasisha watanzania kuongeza uzalishaji katika kilimo ili serikali itoe mikopo ya matrekta. 

Mhe Mwanjelwa alisema kuwa mafanikio ya mpango huo ni makubwa kwani Katika Wilaya ya Manyoni uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kufikia Tani 42,554 katika msimu wa mwaka 2015/2016 ambapo uzalishaji wa mpunga umeongezeka kutoka Tani 1342 mwaka 2011/2012 hadi kufikia Tani 6212 mwaka 2015/2016.

Alisema kwa upande wa Zao la Alizeti uzalishaji umeongezeka kutoka Tani 4464 mwaka 2010/2011 hadi kufikia Tani 21,871 mwaka 2016/2017 wakati huo huo zao la Ufuta uzalishaji umeongezeka kutoka Tani 2285 mwaka 2010/2011 hadi kufikia Tani 8874 katika msimu wa mwaka 2015/2016.
Aliongeza kuwa katika Mkoa wa Singida uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka Tani 453,297 mwaka 2013/2014 hadi Tani 481,452 mwaka 2015/2016.

Uzalishaji wa mazao ya biashara umeongezeka kutoka Tani 184,066 mwaka 2012/2013 hadi kufikia Tani 293,873 katika msimu wa mwaka 2015/2016.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mhe Mary Mwanjelwa alisema kuwa Jumla ya Matreka yanayofanya kazi nchini ni 18,774 ambapo kati yake Matrekta makubwa ni 11,500 na matrekta madogo ya mkono ni 7274.

Alisema kuwa Wilaya ya Manyoni pekee ina jumla ya matrekta makubwa 32 Matrekta madogo ya Mkono 39 na wanyamakazi 14784 yanayotumika katika kuongeza ufanisi wa kilimo ambapo pia kilimo cha kutumia Maksai ni maarufu katika Wilaya hiyo.
Alisema kuwa pamoja na jitihada za serikali kuu katika kuhakikisha wakulima wanapata zana bora za Kilimo Halmashauri za Wilaya kote nchini zimelekezwa kuhamasisha wakulima kujiunga au kuanzisha vyama vya akiba na Mikopo (SACCOS) ambavyo vitakopesha wanachama wake au kuwadhamini kupata mikopo kutoka kwenye Taasisi za fedha kwa ajili ya kununua Zana hizo bora za Kilimo ikiwemo Matrekta.

Akijibu swali la Nyongeza la Mbunge Masare aliyetaka kufahamu namna ya kupatiwa mikopo kwa wananchi ambao hawajajiunga na vyama vya akiba na mikopo (SACCOS), Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa alisema kuwa sifa ya wananchi kukopeshwa ni pamoja na kujiunga na Vyama Vya Ushirika lakini pia Wizara ya Kilimo kupitia Mfuko wake wa Taifa wa pembejeo za kilimo ataruhusiwa mkulima mmoja mmoja kukopa jinsi atakavyo kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
MWISHO

Friday, 3 November 2017

Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji akizungumza katika mkutano wa Global Business Forum 2017 kuhusu Viwanda kwa Nchi za Afrika, mkutano huo wa siku mbili umefanyika Dubai, UAE na kuhudhuriwa na watu 5860 wakiwepo viongozi wa serikali za nchi za Afrika na wafanyabiashara. (Picha na Clouds Media)
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group), Mohammed Dewji amepongeza uamuzi wa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kufufua viwanda ambavyo vilikuwa havifanyi kazi.

Dewji ametoa pongezi hizo wakati akizungumza katika mkutano wa siku mbili wa Global Business Forum 2017 (GBF) kuhusu Viwanda kwa Nchi za Afrika uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).

Mfanyabiashara huyo ambaye anamiliki viwanda 41 alisema uamuzi aliochukua Rais Magufuli ni mzuri hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati.Dewji alisema kampuni yake ya MeTL Group itaendelea kushirikiana na serikali na katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo amejipanga kuhakikisha anatoa ajira kwa Watanzania 100,000 jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi wa nchi na kwa wananchi..

 “Nianze kwa kumpongeza Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa shabaha yake ya viwanda, ni nzuri sababu kuna ongezeko la thamani lakini pia watu wanaweza kupata ajira na pia hizi biashara zitalipa kodi ambazo zitaisaidia serikali kuwekeza kwenye mambo ya afya na maji na huduma za jamii. Mimi shabaha yangu kwenye miaka saba au nane ijayo MeTL Group tunataka tuajiri watu 100,000,” alisema Dewji.

Dewji ambaye kwa mujibu wa jarida la Forbes ni tajiri namba moja nchini aliongeza kuwa utendaji wa Rais Magufuli ni wa kasi hivyo anategemea kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo uchumi wa Tanzania utakuwa umekuwa  sana.

“Mimi naona kwa kasi ya Mhe. Rais kwenye miaka miwili au mitatu ijayo tutakuwa tumefika mbali sana, uchumi wetu kwasasa ni asilimia sita au saba lakini kama tukitaka kuondoa umaskini lazima nchi yetu ukuaji wa uchumi uanze kukua kwa zaidi ya asimilia 10, mimi nina muamini sana Mhe. Rais na shabaha yake kwahiyo Mungu atutangulie na sisi tupo nyuma yake tutafika hivi karibuni,” alisema Dewji.

Pia Dewji alizungumzia umuhimu wa mkutano wa GBF ambao umekutanisha watu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika wakiwepo viongozi wa serikali za nchi za Afrika na wawekezaji alisema ni nafasi ya kipekee kwani pamoja na kujadili viwanda pia amepata nafasi ya kuwaelezea washiriki wa mkutano fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini.

“Umuhimu ni mkubwa sana nakuja hapa kama MO lakini pia nawakilisha nchi yangu Tanzania, nimeitangaza nchi yangu ili watu waje na wawekeze, nimewaeleza mazingira yetu ya uwekezaji ni mazuri, tuna malighafi na tunahitaji viwanda angalau watu wetu wa Tanzania wapate ajira na serikali ipate kodi,” aliongeza Dewji.

Wednesday, 18 October 2017

Msanii Kala Jeremiah akitumbuiza kwenye Kongamano la Uzinduzi wa Mabaraza ya Vijana Jijini Mwanza, lililofanyika uwanja wa Furahisha jumapili Oktoba 15,2017.

Binagi Media Group
Kongamano hilo liliandaliwa na taasisi ya Youth & Environment Vision ya Jijini Mwanza kwa kushirikiana na taasisi ya Umoja wa Mataifa ya UNA Tanzania, The Foundation for Civil Society pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo Cocacola, TCRA, pepsi na Tecno.

Mgeni rasmi alikuwa Kaimu Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, William Mnyippembe ambaye aliwasisitiza vijana kujitambua kama ambavyo sera ya taifa ya vijana ya mwaka 2007 inavyosisitiza kwa kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo.

Aidha aliwataka kutumia vyema mitandao ya kijamii na kujiepusha na usambazaji wa jumbe zizizo na maadili katika jamii ikiwemo jumbe za uchochezi ambapo kongamano hilo liliwahusisha pia vijana kutoka shule mbalimbali Jijini Mwanza.

Mkurugenzi wa taasisi ya Youth & Environment Vision, Jonathan Kassib alisema kongamano hilo lililenga kuwahamasisha vijana kuunda na kujiunga na mabaraza ya vijana katika mitaa yao kwa ajili ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili ikiwemo kutumia fursa zinazowazunguka kupitia fedha za asilimia tano zinazotolewa na halmashauri kupitia mapato ya ndani.

Afisa Miradi kutoka UNA Tanzania, Saddam Khalfan alitoa wito kwa vijana kutilia maanani yale yanayopewa kipaumbele kupitia sera yao ya taifa kwa vijana na pia kuwa mstari wa mbele kujitafutia taarifa za kisera kwa ajili ya maendeleo yao.
Mgeni rasmi Kaimu Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, William Mnyipembe (kushoto) akizungumza kwenye kongamano hilo. Kulia ni Afisa Miradi UNA Tanzania, Saddam Khalfan.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mkolani wakitumbuiza kwenye kongamano hilo
Wanafunzi waliofanya vizuri kwenye michezo wakipokea zawadi kwenye kongamano hilo
Washindi wa michezo mbalimbali wakipokea zawadi kutoka kampuni ya simu ya Tecno
 Mkurugenzi wa Miradi wa Tacosode, Theofrida Kapinga akizungumza jambo wakati wa semina iliyofanyika katika ukumbi wa valentine mkoani Iringa
Afisa mchechemzi wa mradi Abrahm Kimuli akiendelea kutoa elimu kwa wanasemina walikuwa wamehudhuria katika ukumbi wa valentine
 Baadhi ya washiriki wakiwa kwenye mijadala ya sekta ya afya na jinsi gani wanaweza kutatua changamoto zinazoweza kuikoa sekta ya afya hapa nchini


Na Fredy Mgunda,Iringa.

BARAZA la Vyama vya hiari na Maendeleo ya Jamii (TACOSODE) limesema wananchi wamekuwa na uelewa kuhamasisha bajeti kuwa na kipaumbele kwa changamoto zinazowakabili.

Hayo ameyasema Mkurugenzi wa Miradi wa Tacosode, Theofrida Kapinga wakati akizungumza semina ya kujadilia jinsi gani ya kutatua changamoto zinazoikumba sekta ya afya iliyofanyika katika ukumbu wa valentine Manispaa ya Iringa.

“Unajua zamani wananchi hata viongozi wa sekta ya afya walikuwa wagumu kuelezea changamoto zinazowakabili lakini saizi wananchi na viongozi wamekuwa na elimu ya kutosha juu ya kueleza changamoto zilizopo katika sekta hiyo ndio maana vitu vingi vinaibuka muda huu” alisema Kapinga

Kapinga alisema licha ya serikali kufanya juhudi kutatua changamoto ili kuto huduma ya afya bora lakini bado sekta hiyo inaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

“Ukiangalia tafiti nyingi zinaonyesha kuwa serikali imekuwa ikishindwa kuongeza bajeti ya sekta ya afya ili kufikia asilimia 15 ya bajeti yote ya serikali kwa kuzingatia azimio la Abuja” alisema Kapinga

Aidha kapinga alisema kuwa moja ya changamoto kubwa ni uhaba wa kupatikana kwa dawa muhimu,vitendanish na vifaa tiba kulinganisha na utafiti wa mwaka 2012 ulifanywa na taasisi ya afya ya Ifakarana kugundua kuwa asilimia 41 ya dawa muhimu zinahitajika kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake afisa mchechemzi wa mradi Abrahm Kimuli aliwataka watumishi wa sekta ya afya kuzibaini changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi kushirikiana na serikali panoja na sekta binafsi.

“Unajua kweli kuna changamoto nyingi ambazo zinawakabili hivyo ni lazima muwe wabunifu kuzitafutia ufumbuzi lakini kwenye hizi sekta binafsi kuwa wasomi wengi ambao wanaweza kutoa ushauri mzuri wa kutatua changamoto zilizopo” alisema Kimuli 

Kimuli alisema kuwa wananchi wamekuwa na uelewa wa maswala ya afya kutokana na elimu waliopata katika mradi wa uhamasishaji wananchi kushiriki katika masuala ya afya katika kuangalia vipaumbele vya bajeti uliokuwa ukitekelezwa katika Mikoa ya Iringa pamoja na Dodoma.

Alisema kuwa wananchi mradi huo katika utekezwaji wake katika Halmashauri ya Iringa pamoja na Kongwa mkoani Dodoma wananchi wamekuwa na mwamko katika masuala ya afya ushiriki kwa kuchangia katika huduma za afya.

Kimuli alisema kuwa mradi huo wa miaka minne umekuwa na matokeo katika wilaya ambazo umetekelezwa kwa wananchi kuwa na mwamko katika masuala ya huduma za afya kwa kuchangia hata nguvu zao pale panapobidi.

Aidha amesema kuwa mradi huo ukiisha wanaweza kufanya katika sekta zingine ili kuwa maendeleo ya katika masuala mbalimbali kutatuliwa.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Iringa Abel Mgimwa alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imejipanga kuahakikisha changamoto zinatatuliwa kimkakati kulinga na bajeti wanayokuwa wameipanga.

“Ukiangalia bajeti ya mwaka wa fedha mwaka huu imepanda hivyo ni dalili njema za kuanza kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikidumu kwa miaka mingi na kuwaomba wananchi na viongozi kuwa na subira katika kipindi hiki cha utatuzi wa changamoto hizo” alisema Mgimwa

Mgimwa aliwapongeza TACOSODE kwa mchango wao katika sekta ya afya ambayo imekuwa na changamoto nyingi hivyo sio rahisi kwa serikali kutatua kwa haraka hivyo.

SPORTS UPDATE

Elimu

NENO

MAKALA

SIASA

DINI

CHEKA

BURUDANI