Saturday 11 October 2014

SUMAYE ATOA DAWA YA UFAULU

By    
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, amesema dawa ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi ni kuboresha elimu kwa kuboresha wafundishaji na ufundishaji.

Sumaye alitoa kauli hiyo jana mkoani Singida katika maadhimisho ya siku ya Walimu Duniani iliyoanzishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Alisema taifa lolote linalopenda kwenda kwa kasi kubwa katika maendeleo ni lazima liweke kipaumbele kinachostahili katika elimu kama zilivyofanya nchi ya Marekani, baadhi ya nchi za Ulaya, Japan, Korea ya Kusini, India na China.

Sumaye alisema kuwaboresha walimu kwa kuwa na idadi inayotosheleza fani zinazofundishwa shuleni, wenye elimu inayotosheleza kufundisha na wanaofurahia kazi yao ya kufundisha.

Alisema jingine muhimu ni kuwatengea maslahi ya kuridhisha na kuwawekea mazingira mazuri ya kazi kadiri inavyowezekana.

Sumaye alisema kuwa na walimu wengi wasio na uwezo wa kufundisha hakutaboresha elimu na kuwa na walimu wengi wenye elimu na ujuzi mzuri lakini wamekata tamaa hakutaboresha elimu.


“Tusije tukafanya kosa kubwa la kufikiri tunaweza kurekebisha kasoro hizi kwa kucheza na viwango vya alama za kufaulu wanafunzi. Huko ni sawa na fikra za mbuni kuficha kichwa chake ndani ya mchanga na kudhani kuwa sasa maadui zake hawamuoni wakati mwili wake mkubwa wote uko nje” alisema.

Sumaye alisema nchi nyingi za Afrika kwa sehemu kubwa zimebaki nyuma kwa sababu ya kutotoa kipaumbele katika elimu na hazijasomesha vijana wao wa kutosha.

Aliongeza kuwa nchi hizo zimekuwa zikitoa elimu isiyokidhi viwango ili mradi kutimiza madarasa na wakati mwingine zimewasomesha vijana bila dira wala malengo hivyo kutokuwatumia ipasavyo.

Sumaye alisema elimu ndiyo inayofanya tofauti katika maisha ya mtu na mtu au nchi na nchi na katika ulimwengu wa kisasa wa utandawazi umuhimu huo wa elimu ni wa dhahiri zaidi.

“Nchi nyingi zilizoendelea zimeweka umuhimu wa pekee katika elimu hasa elimu ya sayansi na teknolojia na nchi ambazo hazitaweka umuhimu unaostahili katika elimu ndizo zitaendelea kubaki nyuma kimaendeleo”.

“Zitaendelea kunyonywa kirasilimali na wenzao waliowekeza katika elimu na zitabaki kuwa soko la bidhaa za wale waliowekeza katika elimu nzuri kwa vijana wao” alisema.

Sumaye alisema ni lazima yafanyike mapinduzi kwenye sekta ya elimu ili yatoe fursa kwa kijana kujiajiri mara anapohitimu mafunzo yake.

0 comments