Wednesday 22 October 2014

UALIMU NGAZI YA CHATI WAONDOLEWA

By    


SERIKALI imefuta rasmi mafunzo ya ualimu ngazi ya Cheti yaliyokuwa yakitolewa katika Vyuo vya Ualimu Daraja la A vilivyopo sehemu mbalimbali nchini. Kufuatia kufutwa kwa mafunzo ya cheti, watakaochukuliwa kwa ajili ya masomo ya ualimu kwenye vyuo vya ualimu wa diploma ni waliopata daraja la tatu na kuendelea na watakapohitimu mafunzo ya miaka miwili ya Diploma (Stashahada) ya ualimu watapangiwa kufundisha kuanzia shule za awali za serikali, msingi na sekondari.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, alisema hayo juzi wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wanajumuiya ya walimu na wanafunzi wa vipaji maalumu wa Shule ya Sekondari Kilakala, Mzumbe pamoja na Wanachuo wa Chuo cha Ualimu Morogoro.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, katika utekelezaji wa mpango mkakati wa kuboresha sekta ya elimu nchini , Serikali imeamua kufuta mafunzo hayo ya ualimu ngazi ya Cheti tangu mwaka huu na kuweka ngazi ya Diploma.

“Kuanzia mwaka huu tumefuta mafunzo kutoa cheti cha ualimu...na tumeweka vigezo vipya vya kujiunga na masomo ya ualimu kwa vyuo vyote vya Serikali na watu binafsi, ni mwanafunzi aliyepata daraja la tatu na kuendelea “ alisema Waziri huyo na kuongeza kusema.

“Vyuo binafsi walishachukua wanafunzi wa ngazi ya Cheti, sasa tumewaambia kuwa mwakani wasiendelee kuwachukua wafuate utaratibu mpya uliowekwa na Serikali,” alisisitiza waziri huyo.

Hivyo aliwataka wanafunzi wanaosoma shule za sekondari nchini kuongeza juhudi za masomo ili wapate ufaulu mzuri utakaowawezesha kuwa na sifa za kujiunga na vyuo vya ualimu ngazi ya Diploma na kuendelea.

Hata hivyo alisema , mwaka huu wanafunzi 4,000 wa kidato cha nne waliofaulu daraja la tatu na la pili kwenye masomo ya sayansi, Serikali imewapatia ufadhili wa kuwasomesha Chuo Kikuu cha Dodoma katika fani ya ualimu wa masomo hayo kwa ajili ya shule za sekondari na msingi.

Kwa mujibu wa waziri huyo, mbali na kufuta mafunzo ya ualimu ngazi ya Cheti, Serikali pia imeanzisha mpango wa kuwaendeleza kimafunzo kazini walimu wa shule za msingi wenye ngazi ya Cheti ili wafikie ngazi ya Diploma.

Hivyo alisema ,awamu ya kwanza ya mwaka huu, Serikali imetenga nafasi 935 kwa ajili ya walimu hao wa cheti waliopo kazini kwa kujiendeleza kwenye Vyuo vya Ualimu vya Diploma ili waendelee kufanya kazi zao za ufundishaji shule za msingi.

“Lengo ni kuboresha viwango vya elimu nchini kuanzia shule za awali za Serikali, msingi hadi sekondari, zifundishwe na walimu wenye Diploma na shahada ya vyuo vikuu.“

Hata hivyo, vyuo vya ualimu vya daraja la A vitaendelea kuboreshwa kimiundombinu ili kuviwezesha kuchukua wanafunzi wa masomo ya ualimu ngazi ya Diploma ili kukidhi mahitaji ya walimu hapa nchini.

Kuhusu shule za vipaji maalumu nchini zikiwemo za wasichana Kilakala na wavulana Mzumbe, waziri huyo alisema , matokeo ya kidato cha nne na sita bado hayaridhishi kulingana na kuitwa kwao shule za vipaji maalumu.
“Shule hizi za vipaji maalumu zinakabiliwa na changamoto ya kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha nne na sita…shule ya vipaji ni kiongozi wa viwango vya ufaulu wa hali ya juu ili zioneshe mfano, zinaposhindwa kushika nafasi za juu hazitoi picha nzuri ya kuitwa hivyo,” alisema Waziri.

Kutokana na kushindwa kufaulisha na kushika nafazi za juu, waziri huyo aliwataka walimu wote wa shule hizo kuongeza jitihada katika ufundishaji na pia wanafunzi kusoma kwa bidii ili matokeo yao yawe bora zaidi kuliko ya shule nyingine za kawaida.

Hata hivyo alisema, Serikali itayashughulikia matatizo na changamoto mbalimbali zinazokwamisha juhudi za kufikia mafanikio bora, kwa kutafuta na kuziwezesha kifedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya majengo, vitendea kazi vya masomo ya kujifunzia na kufundishia na usafiri hasa magari.

“Hili la changamoto za shule kongwe za Serikali sasa jicho letu lipo huko kuziwezesha ili ziwe bora zaidi na moja ni magari na miundombinu mbalimbali ya shule,” alisema Dk Kawambwa.

Katika hatua nyingine, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ualimu Morogoro, Azaria Ndyumyeko, alisema katika mpango wa Diploma ya kawaida elimu ya msingi ya mafunzo kazini (ODPE) mwaka 2014/2015, chuo kilipangiwa walimu 386 wa kujiendeleza na walioripoti ni 157.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, kati ya walimu walioripoti wa kike ni 58 na wanaume 99, na wasioripoti ni 229 na wengi wamekabiliwa na changamoto za waajiri wao ambao ni wakurugenzi wa halmashauri wameshindwa kuwapatia ruhusa.


CHANZO: HABARI LEO

0 comments