Thursday, 11 December 2014

FID Q KUANZISHA KAMPENI YA KUHAMASISHA VIJANA

By    
MSANII wa muziki wa kizazi kipya Fareed Kubanda, Fid Q, amezindua kampeni maalumu ya kuhamasisha uzalendo kwa vijana wa Kitanzania ijulikanayo kama Tuonane Januari.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Fid Q alisema ameamua kuanzisha kampeni hiyo kwa lengo la kuwafikia wanajamii hasa vijana kuwataka kujihusisha kikamilifu katika masuala mbalimbali ya kimsingi.

Alisema vijana mbalimbali wamekosa mwamko katika kujihusisha na masuala mbalimbali ya vijana kama vile kupiga kura kwenye chaguzi mbalimbali na kuendeleza harakati mbalimbali za kimaendeleo.

Aliongeza kwa kuona hali hiyo ameamua kushirikiana na wasanii wengine katika kufanya matamasha mbalimbali ya kuelimisha jamii ambapo ataanza na Njombe.

“Kuna kitu kimoja ambacho watu wengi hasa vijana wenzangu hawakifahamu, nchi yetu ni changa sana. Vijana nchi hii chini ya umri wa miaka 35 ni zaidi ya asilimia 80 ya idadi ya watu, wakati watu wazima zaidi ya miaka 60 ni asilimia chini ya tano ya watanzania wote.

Hizi ni takwimu za sensa iliyopita na hivyo utaona nafasi ya vijana katika mambo mbalimbali hapa nchini,” alisema Fid Q.
Aliwataka vijana kutambua pia nafasi zao katika kubadilisha jamii hasa kwa kutumia nguvu ya kura zao katika kuchagua viongozi bora hasa katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii na uchaguzi mkuu wa 2015.

“Lazima vijana tuamke na tushiriki kikamilifu, kwanza vijana wenye uwezo na sifa za kugombea nafasi za uongozi ni lazima wafanye hivyo, pili vijana wenye vigezo vya kupiga kura pia ni lazima wafanye hivyo maana ni wajibu wetu pia vijana ni lazima tushiriki kikamilifu katika mchakato wa kampeni ili kuhakikisha ishu zetu za msingi zinajadiliwa na wagombea na zinapewa kipaumbele,” alisema.

Katika mkutano wake huo aliongozana na wasanii wengine mbalimbali ambapo kwa pamoja walionesha nia ya kusaidia vijana katika kusaidia jamii.

0 comments