Sunday, 4 January 2015

DIAMOND APEWA CHAVU CAF

By    
NYOTA wa muziki wa kizazi kipya Nassib Abdul ‘Diamond Plutnamz’ anatarajiwa kuburudisha kwenye sherehe za utoaji wa tuzo za wanamichezo bora zinazoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zitakazofanyika Nigeria, Januari 8 mwaka huu.

Kwa mujibu wa ratiba za shoo alizoweka kwenye mtandao wake Diamond, baada ya kufanya shoo kubwa Kigali, Rwanda inayofuata ni hiyo ya tuzo za Glow-CAF.

“Nawashukuru mashabiki wa Rwanda kwa kuniunga mkono katika shoo kubwa katika sherehe za kuukaribisha mwaka, nawapenda wote, sasa najipanga kuelekea Nigeria,” alisema Diamond kwenye mtandao.
Diamond, ambaye alipata mafanikio makubwa mwaka jana kwa kutwaa tuzo nyingi za kimataifa, atafanya shoo hiyo kubwa kisha atarudi Dar es Salaam kufanya nyingine kabla ya kwenda Zanzibar na Mwanza aliko alikuwa kwa ajili ya burudani.

Kwa mujibu wa mtandao wa glowworld, wasanii wengine wa Afrika walioalikwa kutumbuiza ni Hugh Masekela kutoka Afrika Kusini, Flavor wa Nigeria, Fally Ipupa wa Congo DRC, Hakim kutoa Misri, Kikundi cha kwaya cha Pan African kutoka Soweto Afrika Kusini na kundi la P-Square.

Katika tuzo hizo ambazo huandaliwa kila mwaka zaidi ya wachezaji 40 wa Afrika wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi zao, na wale wanaocheza ndani ya Afrika wanawania.

Tuzo zinazowaniwa ni mchezaji bora wa Afrika wa mwaka anayecheza nje, pia anayecheza ndani ya Afrika, timu bora ya taifa ya mwaka, klabu bora ya mwaka na kocha bora wa mwaka.

Nyingine ni timu bora ya taifa ya wanawake, mwanasoka bora wa kike wa mwaka, chipukizi bora, mwamuzi bora, gwiji bora na mchezaji wa jumla.

Wachezaji mbalimbali ambao waliwahi kushinda tuzo hizo ni Samuel Eto’o wa Cameroon mwaka 2005 na 2010, Didier Drogba wa Ivory Coast mwaka 2006 na 2009, Frederic Kanoute wa Mali mwaka 2007, Emmanuel Adebayor wa Togo 2008, Yaya Toure wa Ivory Coast mwaka 2011, 2012 na 2013, anapewa nafasi kubwa pia mwaka huu.

CHANZO: HABARI LEO

0 comments