Monday, 23 February 2015

SERIKALI KUIPA NGUVU NACTE


https://pbs.twimg.com/profile_images/1305593976/nacte_twitter_logo_400x400.jpg

SERIKALI imesema itaendelea kusaidia upatikanaji wa rasilimali watu na fedha ili kuliwezesha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kutekeleza malengo yake ya kukuza stadi na maarifa kwa idadi kubwa ya vijana wanaohitimu shule za msingi na za sekondari.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la mitihani la baraza hilo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema Sekta ya Elimu hususani Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi inakuwa kwa kasi kubwa hasa ikizingatiwa kuwa wahitimu wa ngazi za elimu ya msingi na sekondari inaongezeka kila mwaka.

Waziri Kawambwa alieleza kuwa, wahitimu wengi hawapati fursa za kuendelea na masomo hadi ngazi ya vyuo vikuu.

“Wahitimu hawa wanahitaji fursa mbalimbali za kukuza stadi na maarifa ambazo zitawasaidia kukabiliana na changamoto za maisha yao ya kila siku na kuingi katika soko la ushindani la ajira ndani nan je ya nchi,” alieleza.

Kuhusu ongezeko la vyuo vinavyoendesha mafunzo ya ufundi alisema inaonesha kuwa hadi sasa kuna idadi ya vyuo takribani 501 na kozi zipatazo 1,050 kuanzia ngazi ya Cheti hadi Shahada ya Kwanza zinazoendeshwa katika vyuo kwa udhibiti wa baraza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo, Steven Mlote, alisema ili kuhakikisha vyuo vinazingatia masharti ya usajili wao na vinatoa elimu bora, baraza limeweka nguvu kubwa katika kufuatilia na kusimamia ubora wa elimu unatolewa na vyuo vilivyosajiliwa.

“Baraza limefungua ofisi katika Kanda 6 kwa ajili ya kusogeza huduma mikoani na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji. Aidha, kukamilika kwa jengo hili ni utekelezaji wa mkakati wa kuimarisha huduma za kudhibiti ubora kwa vyuo,” alisema.


CHANZO: HABARI LEO

0 comments