Maendeleo ya Makazi imebomoa nyumba 11 zilizojengwa kiholela bila kufuata utaratibu na sheria za ardhi katika maeneo ya Mbezi Beach, Boko, Tegeta na Ununio.
Waziri wa wizara hiyo, William Lukuvi aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa ubomoaji huo utaendelea katika maeneo yote yaliyojengwa kinyume na utaratibu.
“Kutokana na migogoro mbalimbali ya ardhi na udanganyifu, hii ni kiama kwao kwa sababu kuna watu wanamiliki ardhi kinyume na utaratibu na wanajenga bila kufuata utaratibu,” alisema.
Alisema katika nyumba zilizovunjwa kuna waliofanya utapeli na kumiliki hati bandia na wapo waliowadhulumu wamiliki halali wa viwanja hivyo kutokana na kutokuwa na uwezo.
“Wenye hela wamekuwa wakiwadhulumu wenye hati halali na wengine wanawahamisha watu kutokana na uwezo wao na wanajenga... Watu hao tutawavunjia bila kujali gharama walizotumia hata kama ni maghorofa,”alisema.
Alisema,”wapo wananchi waliopata matatizo ya kudhulumiwa na kama wamefika kwenye ofisi za ardhi wameshindwa kutatuliwa migogoro yao naomba waniandikie barua kwa jina langu ili zinifikie moja kwa moja... Kama umeona mgogoro wako ni sugu niandike barua nitashughulikia suala lako,” alisema.
Aidha alisema anatarajia kuanza ziara mikoani kwa ajili ya kushughulikua tatizo hilo na kusikiliza malalamiko ya wananchi. Katika hatua nyingine, Lukuvi aliwataka wamiliki wa ardhi kuhakikisha wanalipa kodi ya ardhi na kusisitiza kwamba watakaokaidi agizo hilo ardhi zao zitatwaliwa.
Wakati huo huo, serikali imeanza kutekeleza mpango kabambe wa kusimika mfumo funganishi wa kielektroniki kwa ajili ya usimamizi wa sekta ya ardhi kuanzia ngazi ya Taifa, Kanda, wilaya na vijijini unaojulikanna kama ‘Integrated Land Management Information System (ILMIS) ambao unatarajiwa kupunguza migogoro ya ardhi nchini na muda wa kuendesha mashauri ya ardhi.
Mfumo huo ambao unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya ardhi utakapokamilika, miamala yote ya ardhi itafanywa ndani ya mfumo na si vinginevyo ambapo itasaidia kuwa na hati ya kiwanja kwa mmiliki mmoja na si kama ilivyo sasa ambapo kiwanja kimoja kinakuwa na zaidi ya hati moja.
Waziri Lukuvi alisema awamu ya kwanza ya mradi huo itagharimu dola za Marekani milioni 35 na utekelezaji wake utasimamiwa na wizara hiyo kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu.
Alisema utekelezaji wa mfumo huo wa ILMIS utafanyika kwa awamu mbili na utajumuisha ardhi ya mjini na vijijini kama ilivyo kwenye sheria zote mbili za ardhi.
Alisema awamu ya kwanza inakadiriwa kutekelezwa kwa miaka miwili kuanzia Machi 2015 hadi 2016 na itaanza kutekelezwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na Morogoro ambapo itakuwa na uundwaji wa programu ya kielektroniki, kujaribu mfumo katika kanda zilizochaguliwa, marekebisho na mpango wa maandalizi kwa ajili ya kusambaza mfumo.
Alisema awamu ya pili inatarajiwa kuwa na uboreshaji wa mfumo kutokana na matokeo mazuri yaliyopatikana kwenye awamu ya kwanza na kusambaza mfumo nchi nzima na awamu hiyo inatarajiwa kuchukua miaka mitatu kuanzia 2017 hadi 2020.
0 comments