Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala. |
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala (pichani), amesema kero ya ukosefu wa maji kwa Jiji la Dar es Salaam, itamalizika baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa mitatu ya maji ambayo itazalisha lita milioni 700 za maji safi na salama kwa siku.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa wiki ya maji kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc), sambamba na uzinduzi wa mdahalo wa kitaifa wa sera ya maji.
Makala alisema mahitaji ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam kwa siku ni lita milioni 450, lakini uzalishaji kwa sasa ni lita milioni 300 na hivyo kuwa na upungufu wa lita milioni 150.
Alisema miradi ya Ruvu Chini, Juu na visima vya Kimbiji Mpera, itawezesha upatikanaji wa maji kwa siku kwani kutakuwa na uzalishaji wa lita milioni 700 na hivyo kumaliza tatizo kwa Jiji la Dar es Salaam.
Alifafanua kuwa mradi wa Ruvu Chini utazalisha lita 270,000, Ruvu Juu lita 182,000 na visima vya Kimbiji na Mpera vitazalisha lita 248,000.
Makala alisema maji ya Ruvu Chini yanashindwa kutumika kwa kuwa kuna watu wamefungua kesi mahakamani na hivyo kukwamisha ulazaji wa mabomba ya maji umbali wa kilomita tatu hadi kwenye chanzo.
Alisema mradi wa Ruvu Juu wa ulazaji wa mabomba kwa umbali wa kilomita 14, umeanza na utakamilika mwaka huu na hivyo maeneo ya Ubungo na Kimara kuondokana na tatizo la maji.
Alisema kuna changamoto kubwa ya upotevu wa maji kwa kuwa maji yanayozalishwa kwa Jiji la Dar es Salaam yanapotea kwa asilimia 56 kutokana na uchakavu wa miundombinu na wizi wa maji unaofanywa na watumiaji wakubwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Makala amewataka wanachama wa Sadc kuwa na matumizi endelevu ya maji yanayotegemewa na nchi husika ili kulinda vyanzo vya maji ambavyo vingi vinakauka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
"Kutokana na mabadiliko ya tabianchi kadiri siku zinavyosonga mbele, vyanzo vya maji vinapungua kwa sababu ya uharibifu wa vyanzo husika, bila kuwa na matumizi mazuri ya maji vizazi vijavyo vitaishia kuona miundombinu ya maji bila maji," alisema.
Alisema kwa Tanzania idadi ya wanaopata majisafi na salama umeongezeka kutoka watu 300,000 hadi 500,000 mwaka jana na kwamba jitihada mbalimbali zinafanyika ikiwamo kugundua vyanzo vipya.
Mkutano huo umejumuisha wadau mbalimbali wa maji kutoka nchi wanachama, lengo likiwa ni kupata uzoefu na jinsi ya kuwa na matumizi endelevu ya maji ya maeneo ya mipakani.
CHANZO: NIPASHE
0 comments