Thursday 14 January 2016

HESLB WAVUNJA RIKODI

By    

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa jumla ya Sh bilioni 459 kama mikopo kwa elimu ya juu kwa wanafunzi 122,486, wanaosoma katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi katika mwaka wa masomo 2015/2016.

Hiyo ni idadi kubwa zaidi ya wanufaika na fedha kuwahi kutolewa tangu kuanzishwa kwa Bodi hiyo mwaka 2005 na kwa ujumla, katika historia ya utoaji wa mikopo nchini. Fedha hizo zimetolewa kati ya Novemba 2015 na Januari 10, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Meneja Habari, Elimu na Mawasiliano HESLB, Omega Ngole alisema katika mwaka uliopita wa masomo 2014/2015, Serikali kupitia Bodi ilitoa jumla ya Sh bilioni 341 zilizowanufaisha wanafunzi 99,069.

Ngole alisema kati ya fedha zilizotolewa, Sh bilioni 199.7 zinakwenda kwa wanafunzi 53,537 waliojiunga na masomo kwa mwaka wa kwanza Novemba 2015 katika vyuo mbalimbali na Sh bilioni 259.1 zinalipwa kwa wanafunzi 68,916 wanaoendelea na masomo, yaani mwaka wa pili, wa tatu na kuendelea katika vyuo vya umma na binafsi.

Aliongeza kuwa kundi kubwa la wanafunzi waliopata mkopo ni wale wanaosoma programu za kipaumbele, ambazo ni Udaktari wa binadamu, Udaktari wa Meno, Udaktari wa Wanyama, Ufamasia na Uuguzi na Ualimu wa masomo ya Sayansi na Hesabu na Uhandisi wa Umwagiliaji, wengine ni yatima na walemavu.

Aidha, alisema pamoja na mafanikio ya kuwawezesha wanafunzi hao, bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo kasi ndogo ya urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika, hali inayoathiri uwezo wa Bodi kuwakopesha Watanzania wengi zaidi.

“Licha ya changamoto hizo, uwezo wa Bodi katika kukusanya madeni umeongezeka kwa mwaka kutoka milioni 53.6 mwaka 2006/2007 wakati Bodi inaanza kazi hadi kufikia bilioni 21 kwa mwaka 2014/2015 na kwa miezi sita ya mwaka huu wa fedha Julai hadi Desemba 2015, Bodi imekusanya jumla ya bilioni 12.1,” alisema Ngole.

Ngole alisema Bodi hiyo inatoa mwito kwa waajiri katika taasisi za umma na binafsi nchini, kuhakikisha wanazingatia matakwa ya sheria iliyoanzishwa na Bodi inayowataka kuwatambua waajiriwa wao, ambao ni wanufaika wa mikopo kukata sehemu ya mishahara yao na kuwasilisha kwa bodi kama marejesho.

Alisema sheria inawataka waajiri wawatambue waajiriwa walionufaika na kuijulisha Bodi ndani ya siku 28 tangu wapate ajira na sheria hiyo, pia inawataka waajiri baada ya Bodi kuthibitisha kuwa mwajiriwa ni mnufaika, mwajiri anapaswa kuitaarifu Bodi ndani ya siku 30 za ajira yake na kukata makato kutoka katika mshahara wa mwajiriwa na kuwasilisha Bodi ndani ya siku 15 baada ya kila mwisho wa mwezi.

“Waajiri wote wanapaswa kutimiza matakwa hayo ya kisheria na kuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameanza kukagua taasisi za umma kama zinazingatia matakwa haya ya sheria na endapo mwajri atakiuka anaweza kupata adhabu ya faini ya Sh milioni saba au kifungo cha mwaka mmoja,” anaongeza Ngole.

Pia aliwataka wanafunzi walionufaika na mkopo, kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili iwasaidie na wanafunzi wengine na kuwataka wanafunzi waliopo vyuoni na walinufaika na mikopo watumie kwa lengo lililokusudiwa.

Chanzo: Habari Leo

0 comments