Thursday 28 January 2016

TRL KUHAMISHIA SHUGHULI ZAO DODOMA

By    
Kampuni ya Reli Tanzania TRL imetangaza rasmi kuhamishia shughuli zake za usafirishaji kwa muda mjini Dodoma, kuanzia Ijumaa ya Januari 29, hadi pale kazi ya ukarabati wa tuta la reli lililopo kati ya stesheni za Kidete na Kilosa, mkoani Morogoro litakapotengemaa.

Aidha, kuhamishwa kwa shughuli za TRL kwenda Dodoma, kunachangiwa pia na tishio la mafuriko ambalo kwa mujibu wa kampuni hiyo haijulikani yataisha lini.

Kwenye Stesheni ya TRL, Jijini Dar es Salaam, tangazo lililobandikwa katika moja ya kuta zake, linawaarifu wasafiri wanaotumia reli ya kati kuwa shughuli za usafishaji zitahamishiwa Dodoma, lakini taarifa zaidi watazipata kupitia vyombo vya habari.

Na Jumatano ndipo uongozi wa kampuni ukazungumza kuwa shughuli hizo rasmi zitaanza kutokea Dodoma kuanzia Ijumaa hii hadi pale kazi ya ukarabati wa tuta la reli lililopo kati ya stesheni za Kidete na Kilosa, mkoani Morogoro litakapotengemaa.

Kwenye taarifa yake, TRL imewataka wasafirishaji wa shehena kuwa maombi yao yataanza kupokelewa Ijumaa hii, na treni ikitaraji kuanza safari saa mbili za usiku wa Jumanne, Februari 2 mwaka huu.

Kusitishwa kwa huduma kama hii inayotegemewa na idadi kubwa ya abiria, kunatajwa kuchangiwa zaidi na uduni wa miundombinu ya reli

Uongozi wa TRL ulitangaza kusitisha huduma za usafirishaji kuanzia Machi 6 mwaka jana, baada ya eneo la tuta la reli kati ya stesheni za Kidette na Kilosa kuharibiwa na mafuriko ya mvua iliyokuwa ikinyesha wakati huo.

Kwa maana hii, wasafiri watokao mikoa ya dar es salaam na Morogoro, watalazimika kusafiri kwa kutumia mabasi toka maeneo yao, hadi Dodoma ili kuanza safari zao kwenye mikoa inayofikiwa na reli hiyo.

Chanzo: startvtz.com

0 comments