Wednesday 17 February 2016

fastjet yapunguza safari za Kilimanjaro - Nairobi

By    

Dar es Salaam, Februari 17, 2016 - Fastjet imepunguza mtiririko wa safari zake 
kwenye njia ya Kilimanjaro Tanzania na Nairobi Kenya kuanzia Jumatatu Februari 15, 2016.
Fastjet ambao awali walikuwa wanatoa safari za kila siku kwenye njia hii hivi sasa watakuwa wanafanya  safari kutoka Uwanja Ndege wa  Kimataifa wa Jomo Kenyatta hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro mara mbili kwa wiki  siku za Ijumaa na Jumapili tu.
Mabadiliko ya  mtiririko wa safari utazifanya ndege za fastjet kuondoka Nairobi kila Ijumaa na Jumapili saa 5.40 na kutua Kilimanajaro saa 6.40 na safari ya kurudi ndege itaondoka Kilimanjaro saa 7.10 na kutua Nairobi saa 8.10.

Kupunguzwa kwa safari hizo kumetokana na kuwepo kwa mahitaji kidogo miongoni mwa wateja nyakati za wiki kutoka masoko yote mawili ya Kilimanjaro na Nairobi na hivyo kufanya safari za ndege za kila siku kutokuwa nzuri kibiashara  kwenye siku hizo.
Shirika hilo limesema kuwa lengo lake ni kurejesha safari hizo kwenye njia ya Kilimanjaro –Nairobi pindi tu wateja wake watakapohitaji.


Safari za kila siku za  kutoka Dar es Salaam na Kilimanjaro hadi Nairobi zilianza Januari 11, 2016.
Mahitaji ya abiria kwa safari za ndege kwenye njia kubwa ya kibiashara kati ya majiji ya Dar es Salaam na Nairobi   ambayo kwa pamoja  yana idadi ya watu zaidi ya milioni nane yamekuwa ni ya kuridhisha na fastjet iko kwenye mawazo kuwa  ndege moja ni lazima iongezeke kwenye safari kati ya majiji haya miwili katika siku za usoni.

Matokeo ya safari za fastjet kwenda Nairobi kutoka Dar es Salaam yamekuwa ni makubwa ambako kunaelezwa na ukweli kuwa nauli zinazotolewa na mashirika ya ushindani kati ya  nchi hizo mbili zimeshuka kwa  kiwango cha hadi asilimia 40 tangu fastjet waanze safari zake.
Nauli za fastjet kwa kiwango kikubwa zipo chini kuliko zile zinazotozwa na mashirika mengine  kwa safari za moja kwa moja kati ya Nairobi/Dar es Salaam  ambapo nauli zinaanzia dola 80 kwa safari moja.

Nauli hizo hazijumuishi kodi ya serikali ambayo ni dola 49 kuondokea Tanzania na dola 40 kuondokea Kenya na hivyo fastjet kupendekeza wateja wake kufanya maandalizi mapema ili kutumia fursa hiyo ya tozo la nauli nafuu.



Hata hivyo fastjet inasisitiza kuwa  kupunguza safari kwenye njia kati ya Nairobi na Kilimanjaro kunafungua fursa ya kuongeza uwezo kwenye njia za kikanda zilizopo na hali kadhalika uwezekano wa kuzindua  njia nyingine mpya ya kikanda katika siku za karibuni.

0 comments