Wednesday, 10 February 2016

MAFURIKO YAZINGIRA 53000 PWANI

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo.
WATU 53,446 wilayani Rufiji mkoani Pwani, wamekumbwa na mafuriko, hali iliyowafanya wazungukwe na maji na kuhitaji msaada kufuatia mvua za vuli zinazoendelea kunyesha nchini. Aidha, tayari boti mbili za uokozi, zimepelekwa kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kuwaondoa watu hao, waliozungukwa na maji na kuwapeleka sehemu salama.

Akizungumza na gazeti hili kwa kutoka kwenye eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema maji hayo yametoka maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Morogoro.

“Vijiji vingi wilayani humo vimezingirwa na maji na watu wengi waliokumbwa na kadhia hiyo ni wale waliohamia mashambani kwa ajili ya kilimo na kukutwa na maji hayo pamoja na nyumba ambazo ziko mabondeni,” alisema Ndikilo.

Alisema mvua hizo ambazo zilizoanza kidogo kidogo tangu Januari 31, mwaka huu, zimeathiri zaidi kwenye maeneo ya Kata ya Mwaseni, Tarafa ya Mkongo, Tarafa ya Ikwiriri na Kata ya Muhoro.

“Kutokana na athari za mvua hizo hekta zaidi ya 7,000 za mahindi na hekta zaidi ya 8,000 za mpunga zimesombwa na maji na tayari mkoa umewasiliana na Waziri Mkuu kwenye Kitengo cha Maafa kuomba msaada wa chakula tani 1,280 za mahindi,” alisema mkuu wa mkoa.

Aidha, alisema wameteua wafanyabiashara sita kwa ajili ya kununua mahindi na kuyasaga kwa ajili ya chakula, ikiwa ni njia ya kuwasaidia wananchi pia kukabili mfumuko wa bei unaoweza kujitokeza kutokana na hali hiyo.

Katika hatua nyingine, mkoa umeomba tani 10 za mbegu za mahindi na tani tano za mbegu za mtama kwa ajili ya kupanda kukabiliana na athari ya mazao, yalisombwa na maji ya mvua za vuli, ambapo wiki ijayo zitaanza mvua za masika.

Chanzo: Habari leo

0 comments