Tuesday 2 February 2016

MAHAKIMU 500 KUWAJIBISHWA

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othmani
JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohammed Othman ametoa siku saba kwa mahakimu wakazi na mahakimu wa mahakama za mwanzo 508 kujieleza kwa nini wasifunguliwe mashtaka ya nidhamu au kuwajibishwa kwa kushindwa kufikia kiwango cha kesi walizopaswa kuamua.

Pia Jaji huyo, amekiri kuwa bado hali ya Mahakama za Mwanzo nchini ni mbaya kutokana na uchakavu wa majengo lakini pia mahakama zilizopo hazitoshelezi kulingana na mahitaji huku kukiwa na takribani wilaya 23 ambazo hazina Mahakama za Wilaya.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Mwaka wa Mahakama na Utendaji wa Mahakama kwa mwaka jana, Jaji Othman aliwataka mahakimu hao kuwa ni wale wanaosikiliza mashauri katika Mahakama za Hakimu Mkazi, za Wilaya na za Mwanzo.

Pamoja na kutoa siku hizo saba, aliwaagiza Majaji Wafawidhi wa Kanda kuhakikisha wanachambua na kuainisha mahakimu wote walioshindwa kufikia kiwango hicho cha kesi walizopaswa kuamua.

Alisema moja ya mikakati katika sekta hiyo ya Mahakama iliyojiwekea ni kupima utendaji wa mahakimu ili kwenda na kasi ya uwajibikaji kama ilivyo kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ‘Hapa Kazi Tu.’

Alisema kwa mujibu wa mkakati huo wa kupima uwajibikaji wa kila hakimu na kila kiwango cha Mahakama, idadi ya mashauri anayopaswa kusikiliza hakimu mkazi na wa wilaya ni 250 wakati hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ni mashauri 260 kwa mwaka.

Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa taarifa ya utendaji wa Mahakama kwa mwaka jana, imebainisha kuwa Mahakimu wakazi kwenye Mahakama za Hakimu Mkazi na za wilaya 121 waliamua mashauri chini ya 100. Aidha, alisema mahakimu wakazi na Mahakama za Mwanzo 387 waliwajibika chini ya kiwango.

“Ukiondoa wale walioajiriwa hivi karibuni, wanaofanya kwenye Mahakama za Mwanzo zisizo na mashauri mengi na wale waliokwenda masomoni au likizo za ujauzito, waliobakia wachambuliwe, waanishwe na kujieleza kwa nini hawakufikia viwango hivyo,” alisisitiza Jaji Othman.

Alisema endapo itabainika mahakimu hao hawakuwajibika ipasavyo bila sababu zozote, watafikishwa kwa Kamati ya Mkoa ya Nidhamu na Maadili ya Hakimu na kufunguliwa mashtaka ya nidhamu na mashtaka hayo yatashughulikiwa haraka na Kamati za Maadili za Mahakama.

Alisema mahakama haitowavumilia mahakimu wanaobembeleza kesi huku mahakimu wengine wakiwajibika kwani wananchi wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu wakitaka kasi iongezeke ya kusikiliza mashauri. “Hatua hizi ni muhimu katika mazingira ya sasa ambapo kuchapa kazi na uwajibikaji ni kaulimbiu ya utumishi wa umma.

Mahakimu wasiofikia malengo wamekuwa kama nanga inayozuia jahazi letu kufika kule tunakotaka. Uongozi wa mahakama utang’oa nanga hizo ndio namna pekee itakayowezesha utendaji wa mahakama unaoendana na matarajio ya wananchi,” alisisitiza.

Hata hivyo, Jaji huyo, alibainisha kuwa takribani mahakimu 14 kutoka Mahakama za Mwanzo, walifanikiwa kuamua mashauri zaidi ya 700 ikiwa ni juu ya kiwango, mahakimu 50 waliamua mashauri zaidi ya 500 na mahakimu 150 waliamua mashauri 300.

“Nachukua fursa kuwapongeza mahakimu hao kwa uwajibikaji mzuri kwani katika Mahakama ya Mwanzo Dar es Salaam yupo hakimu aliyeamua mashauri zaidi 922, Dodoma 789 na Arusha 778,” alibainisha.

Aidha, alisema kwa mwaka huo wa 2015, mahakimu waliosikiliza mashauri katika mahakama zote nchini ni 1,240 na idadi ya mashauri yaliyoamuliwa na Mahakama za Hakimu Mkazi, Wilaya na Mwanzo ni 204,073.

Alisema mahakama hizo ziliamua mashauri takribani asilimia 93 mwaka jana kati ya asilimia hizo, asilimia 74.4 ya mashauri yaliamuliwa katika Mahakama ya Mwanzo ambayo kwa sasa ina mahakimu 914 na Mahakama 976.

Pia mahakama za mwanzo zilizotia fora katika kumaliza mlundikano wa kesi na kiasi cha asilimia katika mabano kuwa ni za wilaya za Mkuranga (141), Rufiji (122) na Bukoba Mjini (224).

Akizungumzia maadhimisho ya mwaka ya mahakama, alisema yatafanyika kwa siku tatu kuanzia jana kwa maonesho yenye mafunzo na elimu mbalimbali kuhusu masuala ya mahakama na kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika keshokutwa na kuhudhuriwa na Rais John Magufuli.

chanzo: habari leo

0 comments