Sunday 14 February 2016

MAWAZIRI KUKATWA MISHAHARA KWA AJILI YA UJENZI WA SHULE

RAIS John Magufuli ameagiza kila waziri akatwe Sh milioni moja katika mshahara wake kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa madarasa na shule mpya katika Jiji la Dar es Salaam. Mbali na mawaziri, Rais Magufuli amesema pia yeye, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa watakatwa Sh milioni sita kila mmoja ambazo zitapelekwa katika jukumu hilo.

Amesema hayo jana alipokuwa akizungumza na Taifa kupitia mkutano wake na Wazee wa Dar es Salaam, baada ya kuelezwa changamoto ya ongezeko la wanafunzi wa darasa la kwanza katika mkoa huo, lililotokana na utekelezaji wa ahadi ya elimu bure.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alisema katika mkoa huo sera ya elimu bure imefanya watoto mpaka miaka 11 kutaka kuandikishwa darasa la kwanza, ambao hapo awali walifichwa na kufanyishwa biashara kutokana na wazazi kukosa michango.

Kwa mujibu wa Sadiki, chumba kimoja cha darasa kwa sasa kinakaliwa na wanafunzi 250 hadi 300 na wengine wanasoma nje au kwa awamu, kwani mkoa ulikuwa na lengo la kuandikisha wanafunzi 68,820, lakini mpaka juzi walikuwa wameandikisha wanafunzi 80,276.

Kutokana na changamoto hiyo, alisema wamepanga kujenga madarasa 500 katika mwaka huu wa fedha pamoja na shule mpya. Sadiki alisema wameanza kubana matumizi kwa kuzuia safari za madiwani nje ya nchi, ambazo zimefutwa na wamefanikiwa kuokoa Sh bilioni 4.6 ambazo zimeelekezwa katika elimu ya msingi.

Chanzo: Habari leo

0 comments