Thursday 4 February 2016

SHEKHE PONDA ATOA NENO JUU YA KURUDIWA UCHAGUZI WA ZANZIBAR

By    

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, ameibuka kupinga kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar na kumkumbusha Rais Dk.  John Magufuli, atimize kwa vitendo ahadi aliyoitoa bungeni ili kunusuru visiwa hivyo kutumbukia kwenye uhasama.

Msimamo wa taasisi hiyo umetolewa siku moja baada ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoa wa Dar es Salaam, kutoa tamko la kuunga mkono kurudiwa kwa uchaguzi huo mwezi ujao.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, juzi alisema kurudiwa kwa uchaguzi huo ndio njia pekee ya kumaliza mgogoro wa kisiasa visiwani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Sheikh Ponda alisema uchaguzi uliofanyika mwaka jana kwa pande zote za Muungano uliosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC),  ulikuwa mzuri, huru na haki kwa mujibu wa ripoti za waangalizi.

Alisema  Rais  wa Muungano, wabunge na madiwani walipatikana kwa uchaguzi huo na sehemu ya Zanzibar wabunge wa Bunge la Muungano, walipatikana katika uchaguzi uliosimamiwa na ZEC na matokeo yake wanayaheshimu.

“Kwa sababu ambazo hazina msingi wowote, mwenyekiti wa ZEC alifuta uchaguzi wote wa kuwapata viongozi wa Zanzibar, hatua ile haikuwa halali kwa sababu mbili Kuu, moja ni  Tume baada ya kutoa matokeo haina mamlaka kisheria kufuta matokeo,” alisema na kuongeza:

“Uamuzi wa kufuta matokeo hata kama Tume  ingekuwa na mamlaka, maamuzi yale hayakuwa ya tume bali ni maamuzi ya mtu mmoja,” alisema.

Sheikh Ponda alisema kwa sababu hizo uchaguzi wa Zanzibar na matokeo yake, bado ni halali na kuurudia ni kosa na ni kupanda mbegu mpya ya chuki miongoni mwa wananchi.

Aliongeza kuwa wanaunga mkono hatua za mwanzo zilizochukuliwa kunusuru hali ya kisiasa, kwa kufanya mazungumzo baina ya vyama hasimu vya CUF na CCM.

Kadhalika alisema wanaunga mkono ahadi ya Rais Magufuli, aliyoitoa bungeni ya kushughulikia mzozo huo kwa kushirikiana na mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad , na Rais Dk. Shein kupata suluhu.

“Mpaka sasa Watanzania hatujaambiwa kwa taarifa ya pamoja kutoka CCM na CUF, mazungumzo waliyofanya yameishia wapi yepi wamekubaliana na yepi hawajakubaliana na nini hatma ya mazungumzo yao,” alisema.

 “Tunapinga vikali uamuzi wa ZEC kutangaza tarehe ya kurudia uchaguzi kabla ya ufumbuzi wa mambo ya msingi na ya kisheria kupatikana, hatua hiyo inaweza kuleta fujo hasama na kuharibu utangamano uliopatikana kwa kipindi cha miaka ya karibuni Zanzibar,” alisema.

Alisema ushauri wa Jumuiya kwa Rais Magufuli ni kutekeleza kwa vitendo ahadi yake ili kuhakikisha mzozo huo unapatiwa ufumbuzi  bila kuitumbukiza Zanzibar kwenye uhasama.

CHANZO: NIPASHE

0 comments