Sunday 10 April 2016

WANAOMILIKI MIGODI WATAKIWA KUACHA KAZI SERIKALINI

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka maofisa madini wa kanda, mikoa na wilaya wanaomiliki vitalu vya madini au migodi, waache kazi serikalini.

Mbali na agizo hilo, pia amesema wizara yake haikatazi mafunzo nje ya nchi yakiwa ya muhimu, lakini haiko tayari kukumbatia mafunzo ya muda mfupi yanayotumika kujaza CV kwa semina ya mwezi mmoja au wiki.

Muhongo alisema hayo juzi wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo na kuhoji kwa nini wafanyakazi hawakusanyi maduhuli ya Serikali kwa wingi na haraka, licha ya kuwepo wakuu wa kanda na watendaji wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA).

“Kujaza CV eti semina ya mwezi mmoja au wiki hakuna kwa sasa ni vema kumuita mtaalamu kutoa mafunzo kwa wengi hapa hapa nchini,“ alisema.

Alisisitiza kuwa nchi inataka wataalamu wengi katika sekta muhimu ya gesi na mafuta na matarajio ni kwa miaka 10 kuwe na wataalamu wasiopungua 500 watakaosoma ndani na nje ya nchi.

Alisema pia ameomba nafasi 20 za masomo kila mwaka kuanzia mwakani kwa ajili ya wataalamu wa makaa ya mawe, kwani nchi ilikuwa na mtaalamu mmoja tu ambaye pia amestaafu.

Kuhusu watendaji wa wizara kumiliki vitalu vya uchimbaji au migodi, Profesa Muhongo alisema kitendo kinasababisha kukosekana kwa haki katika usimamizi.

“Kwa hiyo azimio mnalopaswa kuweka leo ni kuwa ofisa wa madini akionekana na vitalu vya madini au mgodi, aache kazi aende kwenye uchimbaji madini. Hawezi mtu mmoja awe na vitalu au migodi halafu awe msimamizi,” alisema.

Alitaka watendaji wake wakuze pato la Taifa kupitia sekta ya mdini kwa kuacha kung’ang’ania uchimbaji madini wa aina moja, bali wajitahidi kuongeza wachimbaji wa kati zaidi ya 20 na wadogo zaidi ya 100.

Aliwataka maofisa wa madini kanda, mkoa na wilaya kuacha ukiritimba ili leseni zitoke haraka na kuacha upendeleo, ili wachimbaji wawe wengi huku akitaka waache kushika maeneo ya madini.

“Jadilini kwa nini tanzanite inatoroshwa kupitia Kenya huku nchi hiyo (Kenya) na India wakiwa wauzaji wakubwa wa madini hayo wakati hawana madini hayo na mtachukua hatua zipi,” alisema huku akitaka kuachana na wimbo wa kuongeza thamani ya madini kwani kwa miaka 10 suala hilo limezungumzwa bila vitendo.

Chanzo: Habari leo

0 comments