Tuesday, 27 August 2013

MAHKAMA YA KADHI HAIPINGIKI

Na David John

BARAZA Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, limesema kipengele cha uwepo wa Mahakama ya Kadhi kwenye Katiba Mpya, hakiepukiki hivyo ni wajibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kuhakikisha Waislamu wanapata haki yao ya msingi.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Shekhe Mussa Yusufu Kundecha, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano waliouitisha ili kupitia Rasimu ya Katiba Mpya ulioshirikisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Alisema Mahakama ya Kadhi ni jambo muhimu kwa Waislamu hasa katika eneo la mirathi na mambo mengine ambapo awali waliwasilisha ombi hilo kwa Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji mstaafu Joseph Warioba kabla rasimu hiyo haijatoka.

"Tu l i p e n d e k e z a k uwe p o kipengele cha kuitambua mahakama hii kwenye Katiba Mpya lakini kinyume na hapo, tume imekataa mapendekezo yetu...tunatarajia kuyapeleka tena kwa tume husika ili katiba iweze kuleta matumaini ya Watanzania wote," alisema.

Naye mjumbe wa baraza hilo kutoka Temeke, Dar es Salaam, Shekhe Abubakar Shabani alisema, watahakikisha suala hilo linapigiwa kelele ili liweze kuingizwa katika Katiba Mpya.

Alisema hata ombi lao la kutaka siku ya Ijumaa iwe mapumziko pia limekataliwa na tume hiyo kama ilivyo Jumapili kwa Wakristo hivyo ni wazi kuwa Waislamu hawatendewi haki.

"Ijumaa ni siku ya ibada kwa Waislamu hivyo inastahili iwe ya mapumziko kama ilivyo Jumamosi na Jumapili, kama haiwezekani Serikali ichague siku nyingine ya mapumziko ambayo itakuwa inatendeka haki kwa pande zote," alisema Shekhe Shabani.

Aliongeza kuwa, pendekezo lingine ambalo walilipeleka kwa tume hiyo ni kuruhusiwa kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu Duniani (OIC), lakini imekataa mbali ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Benard Membe kusema suala hilo halina tatizo lolote kwa Waislamu.

0 comments