Wednesday 15 January 2014

PROF. MAGHEMBE AIPONDA TANESCO, ASEMA IMEJAA URASIMU MTUPU, ATAMANI IPATE MPINZANI

WAZIRI wa maji, Prof Jumanne Maghembe ameelezea kukerwa kwake na shirika la umeme nchini (TANESCO) kwa madai limeshindwa kufikisha umeme vijijini na hivyo miradi ya maji kusuasua.
Kadhalika waziri huyo ametamani kuwapo kwa shirika mbadala ambalo litatoa ushindani kwa TANESCO ili iweze kutekeleza shughuli zake na hivyo miradi ya maji kukamilika kwa watati.
“Tungekuwa na mashirika mengine ya umeme tungeweza kufungiwa umeme haraka, lakini kwa vile ni TANESCO peke 

yake, sasa wananchi hawana maji…. TANESCO, ukiritimba too much,” alisema.
Profesa Maghembe alisema hayo wakati anazindua mradi wa usambazaji majisafi katika kata ya Kiboroloni na viunga vyake, kwani maeneo hayo yalikosa huduma hiyo muda mrefu, huku mipango ya kusambaza katika kata za Ng'ambo na Msaranga ikiendelea.

Alisema wizara yake inatambua kuwa vijiji 74 katika mkoa wa Kilimanjaro havina maji lakini mipango ni kuhakikisha hadi kufikia mwisho wa mwaka huu vinapata huduma hiyo.
Aidha waziri huyo alisema kati ya vijiji hivyo 74, ni vijiji 28 ambavyo miradi yake imekamilika na wananchi wanapata huduma hiyo huku Vijiji 17 miradi yake ipo katika hatua za mwisho lakini tatizo lililopo ni kukosekana kwa umeme.
“Lakini kwa kweli tatizo tulilonalo sasa ni Tanesco…. Kwa muundo walionao ni lazima TANESCO wapandishe soksi zao juu,” alisema.
Alisema hata hivyo vijiji vingine 26 vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya upatikanaji maji na kwamba katika bajeti ya mwaka huu,mipango ni kuvipatia maji vijiji 25 kila wilaya nchini.
Alimtaka mkurugenzi wa mamlaka ya majisafi na majitaka mjini Moshi (MUWSA),Cyprian Luhemeja kuhakikisha hadi kufikia Juni mwaka huu wananchi wote wa Moshi wapate maji.
Naye mkurugenzi wa MUWSA, mhandisi Luhemeja alisema mamlaka imejiwekea vipaumbele Vya kupunguza upotevu wa maji kutoka Asilimia 38 Juni mwaka jana ingawa ilipofika Desemba mwaka jana kiango kilishuka hadi asilimia 24 lengo likiwa kufikia asilimia 9 Desemba mwaka huu.
Vipaumbele vingine ni kuongeza kutoka idadi ya sasa zaidi ya 20,000 hadi 35,000, wamefanikiwa kuongeza chanzo cha coffee curing chenye lita za ujazo wa 1500 huku juhudi za kuchimba kisima katika tanki la Kilimanjaro kitakachokuwa na lita za ujazo 1800 kwa siku zikiendelea.
Alisema mamlaka ilijipa siku 180 kutekeleza mipango yake ambapo walikusudia kukarabati miundombinu na kuondoa mtandao mbovu wenye urefu wa Km 85 lakini hadi kufikia juzi mchakato wa kuondoa Km 24 umekamilika ambapo vifaa vimeshanunuliwa.
via Lukwangule blog

0 comments