
Dewji, hivi karibuni alitajwa kuwa miongoni mwa watu 10 barani Afrika wenye ushawishi katika biashara na siasa kwa mwaka 2014 na jarida la Forbes la nchini Marekani.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Dewji, alisema bara la Afrika lina rasilimali nyingi ambazo zikitumika vizuri zitawakomboa wananchi wake katika lindi la umaskini.
Aliongeza kuwa watunga sera katika mataifa mbalimbali ya Afrika wanapaswa kutunga na kusimamia utekelezaji wa sera zitakazochangia ukuaji wa maendeleo, ajira na huduma za kijamii.
“Nimefurahi kuwa miongoni mwa watu 10 barani Afrika wenye ushawishi… ninaamini mafanikio haya yametokana na Kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Ltd (MeTL) kutanua wigo wake nje ya nchi.
“Kampuni yetu ipo katika nchi 12 barani Afrika, hapa nchini tumeajiri watu 24,000, katika miaka mitano ijayo tutakuwa tumeajiri watu 100,000 kulingana na tunavyopanua biashara zetu,” alisema.
Dewji, aliongeza kuwa bara la Afrika lina soko kubwa la bidhaa zinazozalishwa humo, hivyo wananchi wa nchi husika ni lazima wajenge utaratibu wa kununua bidhaa husika.
Aliongeza kuwa Tanzania ina fursa nzuri zaidi ya kuuza bidhaa zake nje ya mipaka yake kupitia kwa wafanyabiashara wanaozalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Alisema MeTL imekuwa mfano wa kuigwa katika nyanja ya biashara na inashiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.
“Ninawashukuru sana Watanzania wenzangu pamoja na wapiga kura wangu walioniwezesha kuwa mbunge, ninawaahidi tutaendelea kuzalisha na kukuza soko la bidhaa zetu ili ajira ziongezeke zaidi,” alisema.



0 comments