Sunday, 23 February 2014

Mnyika ang’aka matokeo kidato cha nne

By    
MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amesema kuwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2013 yaliyotangazwa juzi na kuonyesha ufaulu umeongezeka kwa asilimia 15.17, yamedhihirisha tahadhari aliyotoa kuhusu mabadiliko ya viwango vya ufaulu yaliyotangazwa na serikali Oktoba 30, 2013.

Mnyika alisema kuwa serikali kwa baraka ya kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) imeamua kulificha taifa juu ya Matokeo Mabaya ya Sasa. Kwamba wachambuzi wa masuala ya elimu wanapaswa kutoa takwimu za matokeo yangekuwa namna gani iwapo viwango vya awali vya ufaulu vingetumika ili nchi ijue hali halisi kwa manufaa ya wananchi.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alitoa wito Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuweka wazi kwa umma ripoti za uchunguzi zilizoundwa kuwezesha wananchi kuihoji serikali iwapo kupanda huko kwa ufaulu ni matokeo ya kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunza au ni kiini macho cha mabadiliko ya wigo wa alama na madaraja.


CHANZO: TANZANIA DAIMA

0 comments