Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM), limewaonya watu
wanaopenda kwenda kufanya kazi katika nchi nyingine, dhidi ya ongezeko
la mashirika yanayosafirisha binadamu kwa kivuli cha kutoa misaada ya
kibinadamu.
Tayari shirika hilo limetoa orodha ya mashirika 23
bandia 23, yanayojitangaza kuwa yanawatafutia watu kazi katika mabara
ya Ulaya, Asia na Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa za shirika hilo, imebainika kuwa watu hao wanaopata kazi wanaishia katika kunyanyaswa.
Msemaji wa shirika hilo hapa nchini, Husna Tandika
aliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa baadhi ya Watanzania
wameshanaswa katika mtego wa mashirika hayo, yanayotumia mitandao ya
kijamii kujitangaza.
Alisema watu wengi wamekuwa wakiingizwa katika
biashara hiyo kwa sababu ya tamaa ya kutaka kwenda nje ya nchi na kupata
kipato kikubwa, ili kuishi maisha bora.
Baadhi ya mashirika yaliyotajwa kujihusisha na
mtandao wa biashara hiyo haramu ni pamoja na Shirika la Kusajili
Wafanyakazi Australia (AIWR/RP), Muungano wa Taasisi za Kuajiri
Wafanyakazi Canada (CAWRA), Shirika la Kuajiri Wafanyakazi wa Kigeni
Canada (CFWRPA) na Kituo cha Kimataifa cha Kuajiri Wafanyakazi cha
Canada (CIRC).
Katika orodha hiyo pia kuna Chama cha Kimataifa
cha Kuajiri Wafanyakazi (CIWRA), Wakala wa kutafuta Wafanyakazi (CRA),
Mpango wa Kutafuta Wafanyakazi Canada (CWRP), Kamati ya Misaada ya
Wakimbizi (GCRHA) na Mpango wa Kimataifa wa kubadilishana wafanyakazi
(GIEP).
Kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la kuajili
wafanyakazi wa kigeni nchini Canada (CFWRPA), ambalo pia limetajwa
kujihusisha na biashara ya kusafirisha binadamu, watu wote
watakaotafutiwa kazi na shirika hilo nchini Canada watalipwa mishahara
mikubwa na hawatabaguliwa kwa rangi, umri, dini au uraia wao.
Pia, waombaji wanapaswa kuwa na vipaji mbalimbali
na wenye uwezo wa kuzungumza lugha moja kati ya Kiingereza, Kifaransa na
Kihispania.
Hata hivyo, IOM linaseama kuwa mashirika hayo
hudanganya kuwa yanashirikiana na mashirika ya umoja wa mataifa, ili
kuwavutia watu wengi, hasa kutoka barani Afrika.
chanzo: Mwananchi



0 comments