Saturday, 22 March 2014

Serikali yapiga ‘stop’ filamu saba

By    
 http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/03/fisso_7-300x169.jpg
FILAMU saba za wasanii mbalimbali hapa nchini zimezuiwa kuoneshwa katika jamii kutokana na kasoro kadha wa kadha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza, Joyce Fissoo, alisema, mwaka 2011 hadi Juni 2013, filamu 2018 za ndani ziliingizwa sokoni, lakini kati ya hizo, saba zilizuiliwa kuoneshwa katika jamii na 16 zilitakiwa zifanyiwe marekebisho.

Fissoo alisema, hadi sasa filamu 14 zimesharekebishwa na mbili bado.

Alisema, walipokea filamu za nje 208 na tano kati ya hizo hazikuruhusiwa kuoneshwa, mbili zilifanyiwa marekebisho na tatu bado hazijarekebishwa.

Alionmgeza kuwa kuanzia Julai 2013 hadi Februari mwaka huu, hakuna filamu ambayo imetakiwa ifanyiwe marekebisho.

“Tunapokuta filamu ina matatizo, tunamwita aliyetengeneza na kukaa naye na kuipitia ili kujua ni maeneo gani yaliyokosewa na kumwambia ayafanyie marekebisho,” alisema.

Katika hatua nyingine, Fissoo aliwataka watengenezaji wa filamu kutumia majina ya Kiswahili kwenye kazi zao, kwani soko kubwa la wanunuzi wa filamu ni Watanzania ambao wanatumia lugha hiyo.

“Kama filamu zetu zitatumia lugha hiyo ipasavyo, tutaikuza, lazima tuwe na uzalendo wa kuipenda nchi yetu,” alisema.

Naye Kaimu Msemaji wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Concilia Niyibitanga, alisema watengenezaji wa filamu wanatakiwa kufuata kanuni za Sheria ya Filamu, ambazo zinaelekeza kwamba, mtu anayetaka filamu ni lazima apate kibali kutoka katika bodi pamoja na mambo mengine.

“Wanatakiwa kupata vibali vya matumizi ya vifaa na mavazi rasmi yanayotumiwa na majeshi ya Ulinzi na Usalama, madaktari, viongozi wa dini na sare za wanafunzi,” alisema.

Aliongeza kuwa wananchi na wasanii wa filamu, wanatakiwa kutoa ushirikiano ili kumaliza tabia ya kunyonywa wasanii, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kununua kazi halali ambayo ina alama ya ukaguzi na stempu za Mamlaka ya Mapato (TRA), ili kukuza uchumi wa msanii na wa taifa kwa ujumla.

0 comments