Thursday, 23 October 2014

WAZIRI- SIMU MARUFUKU KWA WANAFUNZI WA SEKONDARI

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imepigilia msumari kwa kuendelea kuwazuia wanafunzi wa shule za sekondari za serikali za bweni na kutwa kumiliki simu za mkononi wakiwa shuleni na yule atakayekamatwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Licha ya kuendelea kukazia amri hiyo, pia imetoa utaratibu unaowataka wakuu wa shule za sekondari za mabweni kuzitumia ofisi za walimu wa malezi kuwa ni sehemu muafaka ya kuwasaidia wanafunzi wenye matatizo mbalimbali ya kuwasiliana na wazazi na walezi wao.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, jana, wakati alipojibu maswali ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mzumbe, ambayo ni ya wavulana wa vipaji maalumu, ambao baadhi yao walimwomba Waziri aruhusu matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi wa shule za sekondari wakiwa shuleni.

Akijibu swali la msingi la Mwanafunzi Hamis George wa kidato cha sita mchepuo wa PCB, ambaye alisema kuwa hakuna mantiki yoyote kwa wakati huu Serikali kuendelea kupiga marufuku kwa wanafunzi wa sekondari za serikali wa bweni kuwa na simu za mkononi kwani zitawasaidia kuwasiliana na wazazi, walezi nyakati za shida shuleni.

Hoja hiyo ilipingwa na Waziri Kawambwa akisema kuwa maudhui ya uzuia simu za mkononi kwa wanafunzi wa shule za sekondari za Serikali bado halijabadilika na litaendelea kuwepo kutokana na hali halisi ya kimazingira yaliyopo.
“ Hili suala nikiwa Waziri mwenye dhamana , siwezi kulitengua, litaendelea kusimama kama ilivyo, maelekezo ni kwamba wakuu wa shule waandae utaratibu wa kuzitumia ofisi za walimu wa malezi kuwa ni sehemu ya wanafunzi kupeleka matatizo yao yapatiwe ufumbuzi na si kuruhusu mwanafunzi kuwa na simu shuleni,” alisema Waziri huyo.
Hoja hiyo ya kuendelea kupinga marufuku wanafunzi wa shule za sekondari kuwa na simu shuleni, iliungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka, ambaye aliwakata wanafunzi kufuata kile kilichowaleta shuleni, kwani miaka minne ama miwili kwao si mingi wakimaliza wataenda kukumbana na maisha ya kidunia mtaani.
“ Mwanafunzi upo hapa Mzumbe Sekondari kwa ajili ya kusoma...kuwa na simu haikusaidii , kwanza utajipotezea muda kwa kuchati na watu ama marafiki wa kike , mwishowe unafeli mtihani, lawama zitaelekezwa serikalini…vuteni subira mambo haya yanawasubiri baada ya kumaliza elimu yetu ya sekondari,” alisema Mkuu wa Wilaya.


CHANZO: HABARI LEO

0 comments