Saturday, 8 November 2014

BILAL: WAISLAMU PIGENI VITA VIKUNDI VYA UGAIDI

By    

Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal.

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dk Mohammed Gharib Bilal amesisitiza kwamba ni lazima waumini wa dini ya Kiislamu wawe katika sura halisi ya dini hiyo kuliko inavyotafsiriwa katika dunia ya leo na kuhusishwa na ugaidi.

Aliwashauri Waislamu kuwa vikundi vyote kama uamsho, IS, Boko Haramu na al Shabab ambavyo vinabeba sura kwamba eti vinatetea Uislamu, ni vyema vipigwe vita kwa nguvu zote na Waislamu wote duniani kwani vinapotosha taswira na maana halisi ya Uislamu kwa kuwa ni vya hatari na vinaathiri kila mtu wakiwamo Waislamu wenyewe.

Makamu wa Rais alitoa rai hiyo katika hotuba yake ya ufunguzi wa Ijitimai ya Kimataifa jana iliyoandaliwa na Taasisi ya Fiysabilillah Tabligh Markaz katika msikiti mkuu wa Ijumaa ambayo ilishirikisha waumini wa dini hiyo kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Kabla ya kutoa hotuba hiyo, alipata fursa ya kuswali swala ya Ijumaa na mamia ya waumini kwenye Msitiki Mkuu wa Ijumaa uliopo barabara ya Boma, Manispaa ya Morogoro.
Hivyo, aliwataka wanazuoni na Waislamu wote nchini kuwa wana jukumu kubwa la kuungana na wenzao duniani kote kuufanya Uislamu uchukue sura yake halisi.

Pamoja na kusema hayo, Makamu wa Rais aliwashukuru wananchi kwa dua zao njema walizoliombea Bunge Maalumu la Katiba na hatimaye kupata Katiba inayopendekezwa na hivyo akawakumbusha kila mmoja atumie muda wake kuisoma vizuri, kuielewa na kuitathimini katiba hiyo pamoja na kulinganisha na katiba ya sasa.

Hata hivyo, alisema kupitia taasisi ya Fiysabilillah Tabligh Markaz, wamedhamiria kujenga Hospitali kubwa ya Rufaa katika Jiji la Dar es Salaam, na tayari kiwanja kimepatikana eneo la Chamazi na ramani ya michoro ya jengo hilo inaandaliwa ambapo walimwomba Makamu wa Rais awe mlezi wa Taasisi hiyo.


CHANZO: HABARI LEO

0 comments