Sunday, 30 November 2014

MBUNGE AMTAKA SHEIKH WA MKOA KUJITAFAKARI KAMA BAKWATA KIPO KWA AJILI YA WAISLAM

Mbunge wa Konde Khatib Said Haji (CUF) amemtaka Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, kujitafakari na kujipima kama chombo anachokiongoza cha Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kipo kwa ajili ya kuwalinda na kuwasaidia waumini wa dini hiyo au kimegeuka chombo cha kuwatetea wanasiasa hususani wa CCM na serikali yake.

Hivi karibuni Sheikh Salum alikaririwa na gazeti mmoja (siyo NIPASHE), akiwataka Waislamu nchini kumpuuza Mbunge huyo kwani ni mfitinishaji kwa Waislamu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye viwanja vya Bunge, Haji alisema licha ya Bakwata kuwa ni chombo cha kutetea maslahi ya Waislamu na kuwaweka katika masuala ya kiroho lakini kutokana na uongozi mbovu kwa sasa chombo hicho kimegeuka kuwa ni mtetezi wa viongozi wa kisiasa na kuwakingia kifua viongozi wa serikali.

Alisema amelazimika kutoa kauli hiyo kufuatia Sheikh Salum kumwita mbunge huyo mfitini kutokana na kutokubaliana na utendaji wa chombo hicho ambacho kwa sasa kinaonyesha kukiuka maadili ya Bakwata na kujiingiza katika siasa.

"Bungeni niliwahi kusema kuwa Bakwata ni taasisi ya kinafiki kwa waislamu…kauli yangu hii itabaki kuwa pale pale na wala sitoibadilisha," alisema na kuongeza: "Nasema kuwa viongozi wengi wa Bakwata kazi yao kubwa ni kusubiri kupokea kondoo kutoka Uarabuni kwa ajili ya kuchinja huku wakijinufaisha wao viongozi badala ya kuangalia ni jinsi gani ya kuwasaidia waumini wa dini ya Kiislamu."


CHANZO: NIPASHE

0 comments