Wednesday, 24 December 2014

JK AWAPONGEZA DIMOND NA IDRIS

RAIS Jakaya Kikwete amewapongeza mwanamuziki Nassib Abdul 'Diamond' na mshindi wa Shindano la Big Brother Hot Shots, Idris Sultan kwa kuiletea sifa Tanzania kupitia sanaa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari jana, Rais Kikwete alitoa pongezi hizo alipokutana na Diamond Ikulu Dar es Salaam ambapo pia msanii huyo alimwonesha tuzo tano alizoshinda katika mashindano tofauti dhidi ya wasanii wengine wa Afrika mwaka huu.

Pamoja na pongezi hizo kwa Diamond na Idris kwa kile alichosema wameitoa nchi kimasomaso, Rais Kikwete aliwasihi wasanii hao kujihadhari na athari za umaarufu na utajiri katika umri mdogo, zikiwemo kujitumbukiza katika matumizi ya dawa za kulevya na ulevi.

Kikwete amewaasa kuwa ni muhimu kwa wasanii hao kutumia mapato wanayoyapata katika kazi zao za usanii kwa kujijenga kifamilia, ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba zao za kuishi na wanafamilia wanaowategemea pamoja kuwasaidia wasanii wenzao.

"Umaarufu katika sanaa yoyote ile ni wa kupita hivyo tumieni umaarufu mlio nao sasa kama fursa ya kujijenga kimaisha na sio kutumbukia katika kadhia za kidunia kama vile ulevi, ukorofi mbele ya jamii na mambo mengine yasiyofaa," aliwaasa Rais.

Rais Kikwete pia alimpongeza Sultan kwa kuiletea Tanzania sifa na kumtakia mafanikio zaidi katika shughuli zake za baadaye.

Rais Kikwete alisema kuwa Sultan hakuifedhehesha Tanzania kwa kutofanya mambo yaliyo kinyume na maadili ya Mwafrika alipokuwa katika jumba la Big Brother ambapo kwa ushindi wake ametapa zaidi ya Sh milioni 500.

Kwa upande wake, Diamond amemshukuru na kumpongeza Rais Kikwete kwa ushirikiano anaoutoa kwa wasanii nchini, hali ambayo amesema ndiyo iliyowawezesha kupata mafanikio kitaifa na kimataifa.

CHANZO: HABARI LEO

0 comments