Wednesday, 31 December 2014

MKE WA GURUMO APOKEA FEDHA TOKA NSSF

By    
http://m.habarileo.co.tz/images/bajaji-gurumo.jpg
SHIRIKA la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limekabidhi hundi ya Sh milioni mbili kwa mke wa mwanamuziki mkongwe nchini marehemu, Muhidin Gurumo, Mama Pili Gurumo kwa ajili ya Bajaji itakayomwezesha kuendesha maisha yake.

Hundi hiyo ilikabidhiwa jana kwenye ofisi za NSSF Dar es Salaam ikishuhudiwa na viongozi wa Shirikisho la Muziki Tanzania, ambao ndio waliosaidia upatikanaji wa fedha hizo ikiwa ni ahadi yao kwa mama huyo.

Akizungumza wakati anakabidhi hundi hiyo, Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu alisema walipata ombi kutoka katika shirikisho hilo kuwa linahitaji mchango kwa ajili ya kumsaidia mama huyo na wao wakaona watoe kiasi hicho katika kufanikisha ahadi hiyo.

“Walisema wanataka kumnunulia bajaji na sisi tukasema tuchangie kiasi kidogo ambacho kitasaidia sehemu ya mchango huo, kwa sababu NSSF inathamini mchango wa wasanii,” alisema Kintu.

Kintu alisema hakuna Mtanzania ambaye hatambui mchango wa marehemu Gurumo kwani atakumbukwa kwa vile ni sehemu ya ukuaji wa sanaa hiyo nchini.

Kwa upande wa Rais wa Shirikisho la Muziki, Addo Novemba alisema awali waliahidi kuwa wangetafuta wadau kwa ajili ya kumchangia mama Gurumo na mchango huo ni sehemu ya ahadi yao.

Aliwashukuru NSSF kwa kutambua wasanii, huku akisema kuwa wana mpango wa muda katika kuwawezesha wasanii kuchangia kupitia mfuko huo kwa ajili ya kupatiwa nyumba za mkopo.

Novemba alisema kwa upande wao tayari wamemalizana na Mama Gurumo kwani wamemchangia jumla ya Sh milioni 1.1 ambazo walishakabidhi kwa muda. Kwa upande wa Mama Gurumo aliwashukuru NSSF na Shirikisho hilo kwa kumsaidia mchango huo.

Mjumbe mwingine wa Shirikisho hilo mwanamuziki mkongwe, Kassim Mapili aliwashukuru NSSF na kuwaomba wamsaidie dawa za matibabu kwa ajili ya tatizo la moyo ambapo aliahidiwa suala lake kufanyiwa kazi na Shirika hilo iwapo tu kama Shirikisho la Muziki litapeleka maombi.

0 comments