RAIS Jakaya Kikwete amemteua Godfrey Mngereza kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Kwa mujibu wa taarifa ya Basata kwa vyombo vya habari, Rais Kikwete amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa Kifungu namba 5 (1) cha Sheria Namba 23 ya mwaka 1984 iliyolianzisha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Uteuzi huo unaanza Januari 23, mwaka huu. Kabla ya uteuzi huo, Mngereza alikuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Basata kwa kipindi cha kutoka Februari 2013 hadi mwaka huu akitokea Idara ya Utafiti na Stadi za Wasanii ya Basata aliyokuwa akiiongoza kama Mkurugenzi wake.
Mngereza ni msomi mwenye Shahada ya Uzamili (MA) katika masuala ya sanaa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na amepata kuwa Mwalimu wa Chuo Kikuu hicho katika Idara ya Sanaa na Sanaa za Maonesho (FPA) hadi mwaka 2008 alipoajiriwa rasmi na Basata kama Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari ambayo kwa sasa inafahamika kama Idara ya Utafiti na Stadi za Wasanii.
Aidha, shahada yake ya kwanza ilikuwa katika masuala ya sanaa aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.



0 comments