WAISLAMU wametakiwa kuwa na subira wakati viongozi waliopewa dhamana ya kulifuatilia suala la Mahakama ya Kadhi wakifuatilia majibu.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislamu ya Amani Tanzania (TIPF), Sadiki Godigodi katika taarifa yake alisema Waislamu Tanzania nzima wanajua na kutambua viongozi gani waliopewa dhamana kufuatilia suala la Mahakama ya Kadhi na kuwataka Waislamu kuwa na subira na jambo hilo na kusubiri majibu kutoka kwa viongozi husika.
Godigodi alisema taasisi yake inatoa tamko hilo baada ya kujitokeza baadhi ya Viongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu ambao wamekuwa wakizunguka na wanasiasa wa vyama vya upinzani wanaounda Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kupanda kwenye majukwaa jambo ambalo alieleza sio sahihi.
Kwa mujibu wa Godigodi viongozi hao wamekuwa wakiwataka Waislamu wasiikubali Katiba mpya Inayopendekezwa kwa kuwa haitamki lolote kuhusiana na suala la kuwepo Mahakama ya Kadhi na kudai kuwa watazunguka nchi nzima kushawishi Waislamu na Watanzania kuikataa Katiba iliyopendekezwa.
Mwenyekiti huyo wa TIPF aliiomba serikali kuzichunguza taasisi 35 za Kiislamu walizokaa nazo na kukubaliana kuikataa Katiba Inayopendekezwa ili kuzibaini kama zipo kweli au zipo mifukoni na kwamba kupitia tamko hilo TIPF iliomba viongozi wake wa mikoa kuunga tamko hilo.
Godigodi alisema wanaamini suala la Katiba mpya na Mahakama ya Kadhi ni suala nyeti na kwamba linahitaji mtu makini ambaye ni kiongozi mkuu na anayeaminika na Waislamu walio wengi na sio suala la mtu anayetumiwa na Ukawa kuzungumza kama viongozi hao jumuiya na taasisi za Kiislamu.
Aliwataka Waislamu kupuuza matamko ambayo hayana tija kwa taifa na Waislamu, badala yake wafuate maelekezo na matamko yatakayoleta maendeleo kwenye jamii ya Kiislamu na kuachana na watu wanaotafuta umaarufu.
CHANZO: HABARI LEO



0 comments