Sunday 18 January 2015

WATENGENEZA FILAMU NCHINI WALALAMA

WATENGENEZAJI wa filamu nchini wameiomba Serikali isiingilie suala la kujadili bei ya filamu pasipokukutanisha waandaaji wa filamu hizo kwakuwa wao ndio wenye mamlaka na filamu zao.

Katika kikao kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam, waandaaji hao walitaka Serikali kuzuia vikao vyote ambavyo vitaitishwa na bodi ya filamu kwakuwa havizingatii usawa wa kujieleza kwa kila mtu.

Mtayarishaji Chiki Mchoma alisema baada ya soko la filamu kukumbwa na mtikisiko mkubwa, waliamua kutoa jukumu kwa wasambazaji waje na mpango endelevu juu ya kupambana na wizi wa kazi zao.
Alisema ndipo kampuni ya Steps Entertaiment, ilipoamua kujibana na kuagiza vifaa vipya ili kupunguza kuagiza filamu zao kutoka china. 

"Baada ya kuagiza ndipo walipotuambia ili kuendana sawa ni lazima tupunguze bei kwenda sawa na wezi kwakuwa sheria ya nchi imeshindwa kuwabana," alisema Chiki.

Alisema hivyo bei pendekezi ikawa Sh 1,000 kwa wauzaji wa jumla na Sh 1,500 kwa rejareja, wakati zamani ilikuwa Sh 2,000 kwa jumla na Sh 3,000 kwa rejareja.

Naye mtayarishaji wa filamu Mike Sangu, alisema baada ya bei ya filamu kupanda kuna baadhi ya wasanii na wasambazaji wadogo walilalamika. 

Alisema lakini bila wao waandaji wa filamu zenyewe hawakupewa taarifa, walisikia kwamba wasanii na Bodi ya Filamu wamekaa kikao cha pamoja bila ya wao kupewa taarifa wakati filamu wanazojadili ni wao ndio huandaa na wasanii wanakuwa wameshalipwa mapema. 

"Tuliposikia kuna kikao cha pili na sisi kama waandaji wa filamu tulitaka kujua nini kinaendelea, lakini tulipofika tulifukuzwa na kikao kuvunjika," alisema.

John Lister ambaye naye ni mtayarishaji wa filamu nchini kwa muda mrefu, alisema kwa mara ya kwanza wakati soko la filamu linaanza filamu ilikuwa ikiuzwa Shilingi 10,000. Lakini kutokana na soko kuwa gumu bei ilianza kupungua hadi kufikia Sh 2,000, lakini muda wote huo Serikali haikuingilia kwakuwa ni soko huria na kila mtu alikuwa anapanga bei yake

0 comments