Kanisa Katoliki nchini limeanza rasmi mkakati wa kutoa elimu kuhusu Katiba Inayopendekezwa kwa waumini wake, kutokana na kuondolewa kwa mambo mengi ya msingi yaliyotolewa maoni na wananchi.
Mkakati huo umeanzia katika Jimbo la Mwanza ambapo imedaiwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Juda Thaddeus Ruwai’chi ameunda kamati maalumu iliyopewa jukumu la kuchambua na kutoa ufafanuzi juu ya Katiba Inayopendekezwa katika makanisa yaliyopo katika jimbo hilo kupitia semina mbalimbali.
Kura ya Maoni ya kupitisha Katiba hiyo inatarajiwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu (siku 45 kuanzia leo), katika mkakati huo kanisa hilo limeainisha mambo 100 yaliyotolewa maoni na wananchi lakini yakaondolewa.
Uongozi wa kanisa hilo umekiri kuwapo kwa maelekezo hayo yakiwa na lengo la kutoa elimu kwa waumini wake kuhusu mambo yaliyomo na yasiyokuwamo kwenye Katiba Inayopendekezwa.
Kanisa hilo kupitia Tume ya Haki na Amani ya Tec limekuwa linatoa matamko mbalimbali kuhusu mchakato huo, likiwamo lile la Machi mwaka jana la kupendekeza Serikali tatu, lililosababisha Askofu Mkuu wa Jimbo Mkuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kuibuka siku mbili baadaye na kusema msimamo huo siyo wa Kanisa Katoliki nchini.
Katika tamko hilo tume hiyo chini ya Askofu Mkuu wa Tabora, Paulo Ruzoka, CPT ilikuwa imeeleza kuwa muundo wa Serikali mbili haukutatua matatizo ya msingi na badala yake ulilimbikiza kero zilizosababisha Zanzibar kujiundia katiba yake mwaka 2010 bila kushauriana na Tanzania Bara.
Akifafanua tamko hilo siku mbili baadaye, Kardinali Pengo, alisema “Maoni ya Tume hayawezi kuwa ni msimamo wa kanisa. Kanisa Katoliki lina utaratibu wa kutoa misimamo yake na huwa inatolewa na Mwenyekiti wa TEC.”
Kauli ya Rais Tec
Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu mpango huo, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, alisema lengo la mkakati huo ni kuhakikisha waumini wa kanisa hilo wanaijua Katiba Inayopendekezwa ili waweze kukipigia kura kitu wanachokifahamu.
“Kama watapiga kura ya ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’ hiyo ni juu yao wao. Sisi tunachokifanya ni kuwaeleza Katiba hii ina mambo gani,” alisema huku akisisitiza kuwa katiba yenyewe wananchi wengi hawaijui hadi sasa.
Kilichotokea Mwanza Wajumbe watatu wa kamati hiyo wakizungumza katika mkutano uliofanyika katika Parokia ya Nyakato jana walisema kuwa wameombwa na Askofu Ruwai’chi kutoa elimu kuhusu mambo 40 yaliyopuuzwa na kuondolewa katika Katiba Inayopendekezwa.
Chanzo: Mwananchi
0 comments