Taasisi ya Tanzania Islamic Peace Foundation (TIPF), imempongeza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (pichani), kwa jitihada zake kubwa anazozifanya za kukaa pamoja na makundi mbalimbali ya dini na kuyaelimisha kuhusiana na muswada wa serikali kuhusu Mahakama ya Kadhi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TIPF, Sheikh Sadiki Godigodi, alisema kuwa licha ya changamoto mbalimbali anazokumbana nazo, Pinda ameonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa na weledi katika kuyaendea mambo makubwa yanayobeba mustakabali wa taifa.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya jambo zuri sana na la busara sana kwa kukutana na taasisi pamoja na kamati mbalimbali za viongozi wa dini, badala ya kukaa na taasisi moja tu,” alisema Godigodi.
Godigodi alisema suala la Mahakama ya Kadhi ni zito na linawahusu wananchi wa nchi nzima na kuwa haliwezi kubebwa na watu wa mkoa mmoja wala dini moja.
Aidha alisema lazima viongozi madhehebu yote washirikishwe na kusisitiza kuwa jambo hilo Waziri Mkuu amelitekeleza kwa ustadi mkubwa hata kama halitapitishwa na Bunge.
Alisema Pinda ameshafanya jitihada katika mikutano aliyoifanya kwamba inaonyesha dhahiri ana dhamira nzuri kwa Waislamu na Watanzania.
CHANZO: NIPASHE
0 comments