WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali, likiwemo suala la Mahakama ya Kadhi, utawasilishwa katika Bunge lijalo ukiwa na maudhui ya kuangalia jinsi ya kuendesha masuala ya imani ya dini ya Kiislamu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri Pinda alisema Serikali imeridhia kupelekwa kwake baada ya kuwepo na maridhiano baina ya makundi mawili ya dini za Kikristo na Waislamu, juu ya uendeshwaji wa mahakama hiyo.
“Jambo hilo tunalolipeleka bungeni tunataka tuweke utaratibu wa kulitambua kwa kuwa jambo hili linaloombwa na upande wa pili ni la kusaidia utekelezaji wa maamuzi yao na sio kuingilia masuala ya jinai, na ni vyema tuone umuhimu wake,” alisema.
Alisema kati ya muswada huo wenye maeneo 14, Mahakama ya Kadhi ni sehemu ya tano katika sheria hiyo na kwamba mapendekezo yake ni pamoja na kuangalia sheria ya mwaka 1964 inayotamka suala la Uislamu litazamwe na lirekebishwe na kuja na mawazo yatakayoweka vipengele vitakavyowezesha mahakama kuamua mambo yao.
“Serikali imefanya uamuzi huu wa kulipeleka bungeni kwa makusudi kabisa ili kutoa mwongozo mzuri wa mahakama hiyo kuendesha mambo yao ya mirathi, ndoa, talaka vizuri, ila haitashughulika na masuala ya jinai”, alisema Pinda.
Waziri Pinda alisema, katika dini mbili kubwa nchini Wakristo na Waislamu, dini ya Kikristo masuala ya mirathi, ndoa yanaamuliwa kwa urahisi ukilinganisha na masuala hayo kwa upande wa Waislamu, hivyo, uwepo wa chombo kinachowasaidia ni jambo jema.
Alisema awali suala la Mahakama ya Kadhi lilianza miaka mingi lakini kuingia bungeni lilipelekwa na Augustino Mrema na Yusud Rabia (marehemu) ambao walilipeleka mwaka 1998 na kisha kuundiwa kamati iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Arcado Ntagazwa ambaye hoja hiyo ilijadiliwa na kutofikiwa muafaka.
Hata hivyo, alisema Serikali iliendelea kujadili jambo hilo kwa vipindi tofauti na kwa kutumia vyombo mbalimbali ili kufikia mwisho wake na ndipo mwaka 2005 likaingizwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ikisisitiza ufumbuzi wake.
Aidha, aliongeza kuwa Juni mwaka 2009 jambo hilo liliibuka tena wakati Pinda akiwa na wadhifa huo na kuliundia timu ya viongozi wa dini na serikali kuzungumzia muafaka wake na mambo ya msingi yaliyojadiliwa ni pamoja na mahakama hiyo isiingie kwenye Katiba kwa sababu ya utata wake bali lishughulikiwe na dini husika.
Pili, waliona ni vyema uanzishwaji wake ufanywe na dini husika na Serikali itaangalia utaratibu mzuri wa kusaidia utekelezaji wake, na kuwa serikali haitapenda kuingiza masuala ya jinai ndani ya mahakama hiyo.
Na mwisho, walipendekeza jambo hilo liwe la hiari ya waumini na kwamba baada ya hoja hizo, Waislamu walielewa na kusema wataanza wenyewe jambo ambalo limetekelezwa na hadi leo zaidi ya mashauri 300, yameshaamuliwa kwenye mahakama hizo katika mikoa mbalimbali nchini.
“Nilizungumza na Kadhi Mkuu na yeye akaniambia wameshaanza utekelezaji wa uanzishwaji wa mahakama hizo mikoani na hadi leo kesi 300, za miradhi, ndoa, talaka zimeshaamuliwa,” alisema.
Lakini Bunge la Katiba, jambo hilo likaibuka upya kwenye kamati na likaleta utata uliosabibisha jambo hilo kuamulia kwenye kamati ya maridhiano.
Hata hivyo aliongeza, baadaye muswada huo uliharishwa kupelekwa bungeni na Februari 3, mwaka huu kupitia Kamati za Amani ya Dar Es Salaam, yenye wajumbe 50 kutoka pande mbili za Wakristo na Waislamu walikutana na kuzungumzia hilo na kuafikiana.
Na kwamba katika maridhiano hayo, walikubaliana kushirikisha wadau wengi zaidi na ndipo Machi 3, mwaka huu kulifanyika mkutano mwingine wa Kamati ya Maadili na Haki za Binadamu ukiwashirikisha pia dini hizo mbili na serikali.
“Katika mkutano huo walijadiliana na Mwanasheria Mkuu aliyekuwepo na alisema lina nia njema ili mradi Serikali haiingilii,” alisema.
Katika hatua nyingine, Pinda alisema hadi kufikia Februari 26, mwaka huu jumla ya Nakala 1,341,300 za Katiba Inayopendekezwa zilikuwa zimeshasambazwa mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema kati ya idadi hiyo, Zanzibar imepata nakala 200,000 na kwamba lengo lao ni kusambza nakala 2,000,000 na kuwa hizo zilizobaki Serikali imeamua kuzigawa kwa wizara zote, taasisi, asasi, vyombo vya sheria na vyama vya siasa ili kuongeza wigo wa usambazaji kwa wananchi wengi zaidi.
Akifafanua hilo, Pinda alisema utaratibu mzuri unapangwa wa kuangalia jinsi ya kuzigawa mapema hivi karibuni ili kuhakikisha kila chombo husika na makundi yote nchini yanapata nakala hizo, ili wazisome na kuhakikisha wanapigia kura kitu wanachokifahamu.
“Nitoe mwito kwa wananchi, msikubali kurubuniwa, someni mzilelewe, kisha mpigie kura Katiba inayoifahamu,” alisema.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments