Saturday, 14 March 2015

UANGALIFU WAHITAJIKA KATIKA DAWA ZA MENO

By    
Dr. Fenela Mukangara

BAADHI ya dawa za kusafisha meno zinazouzwa nchini zimeelezwa kukosa viwango stahiki vya madini ya fluoride inayotakiwa, jambo linaloweza kusababisha kuongezeka kwa matatizo ya afya ya kinywa na meno.

Aidha, asilimia 45 hadi 50 ya watanzania wameoza meno huku watoto chini ya miaka sita wakioza meno, ikiwa ni sawa na asilimia 60 hadi 70.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Daktari Bingwa na Mtafiti, Profesa Emil Kikwilu wakati akizungumzia kuhusu maadhimishio ya Wiki ya Afya ya Kinywa na Meno itakayoanza kesho.

Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara ataongoza matembezi ya uzinduzi wa wiki hiyo itakayoambatana na utoaji wa huduma mbalimbali za afya ya kinywa na meno kwa watoto waishio katika mazingira magumu na wenye ulemavu wa ngozi.

Kuhusu dawa hizo, Profesa Kikwilu alisema katika dawa zinazotumika kwa ajili ya kusafisha meno zinatakiwa kuwa na madini ya fluoride kwa kiwango cha ppm 1,000 hadi 1,500 ambayo inashauriwa kwa dunia nzima.

Alisema kwa makusudi baadhi ya dawa zimekuwa zikikosa viwango hivyo na kwa kuwa wananchi wengi katika nchi zinazoendelea kwa kutokujua hutumia hadi dawa zenye kiwango cha ppm 200 hadi 300.

“Mwaka jana tulikumbusha kuhusu kuwekwa kwa viwango stahiki vya dawa…ni lazima kila mwananchi kutizama kiwango kinachotakiwa kwa ajili ya afya ya kinywa na meno,” alisema Profesa Kikwilu.

Kuhusu hali ya afya ya kinywa nchini alisema asilimia 30 hadi 35 ya watoto walio na umri unaofikia miaka 12 wameoza meno huku tatizo la fizi likiwa ndio kubwa kwa walio wengi na kusababisha damu kutoka, kuoza kwa nyama za fizi na hata meno kulegea.

Kuhusu wiki ya afya ya kinywa na meno, Rais wa Chama cha Afya ya Meno na Kinywa nchini (TDA), Dk Lorna Carneiro alisema mbali na matembezi pia madaktari wa kinywa na meno watatembelea shule tofauti zenye watoto wenye mahitaji maalumu na kutoa huduma.

0 comments