Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Morogoro, James Mkude alitoa tamko hilo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kusudio hilo la kufanya maandamano hayo Aprili 14, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, maandamano hayo yataanzia ofisi za chama hicho kwenda katika ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa pamoja na Meya ambapo lengo kuu ni kutaka maelezo ya kina kuhusu matumizi ya fedha za mradi wa stendi.
Hata hivyo, alisema maandamano hayo ya kuunga mkono Mbunge wa CCM ni kuushinikiza uongozi wa Manispaa hiyo kutoa majawabu ya msingi ndani ya muda wa siku14 aliotoa Mbunge ambazo zimemalizika jana na chama chao kiliamua kuongeza muda hadi Aprili 14, mwaka huu.
Mbali na kutaka kupata maelezo ya kina kuhusu matumizi ya fedha hizo, pia Chadema kinataka kupata maelezo mengine kutoka kwa uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro akiwemo Meya na Mkurugenzi ili kujua fedha za miradi ya ujenzi wa soko kuu la Morogoro.
Hivi karibuni Mbunge Abood aliyefanya ziara yake kukagua mradi huo unaofanywa kwa pamoja na uongozi wa Manispaa ya Morogoro na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF), kushindwa kutoa taarifa ya matumizi ya fedha hizo licha ya kupewa taarifa za kimaandishi wiki moja kabla na ofisi ya mbunge huyo.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema, mradi huo wa ujenzi wa stendi ya kisasa unaonekana una harufu ya ufisadi miongoni mwa viongozi wa Manispaa, hali inayosababisha kushindwa kutoa taarifa zake kwa mbunge wa Morogoro mjini.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwenendo wa Bunge na Halmashauri nchini wa Chadema, Dk Albanie Marcossy alisema maandamano hayo ni mwendelezo wa operesheni za Chadema za kuelimisha jamii kuhusu matumizi mbalimbali ya fedha za Serikali na kuwataka wananchi kujitokeza.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments