Thursday 16 April 2015

WASIOJUA KUSOMA NA KUANDIKA KUTOINGIA DARASA LA 3


KATIKA kuhakikisha inaondoa kabisa tatizo la watu wasiojua kusoma na kuandika nchini, Serikali imefanya mabadiliko ambapo kuanzia sasa mtoto wa darasa la pili hawezi kuruhusiwa kuingia darasa la tatu kama hajui kusoma, kuandika na kuhesabu ili kuondoa tatizo la watoto wanaomaliza shule ya msingi wakiwa hawajui kusoma.

Pia imepunguza wingi wa masomo katika ngazi za chini kwa darasa la kwanza na la pili ambapo sasa watoto hao watasoma masomo matatu tu badala ya saba, huku ikifuta utaratibu wa walimu na watumishi wengine kulazimika kukubali vyeo kabla ya kuwarekebishia mishahara.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Elimu, Kassim Majaliwa wakati wa ufunguzi wa mafunzo kabilashi ya mtaala mpya kwa walimu wa darasa la kwanza na pili yanayofanyika katika ukumbi wa Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma.

Alisema serikali imeamua kuwapunguzia mzigo wa masomo wanafunzi ili waweze kumudu masomo yao. Pia kwenye sera mpya ya elimu mtoto wa darasa la pili hawezi kwenda la tatu kama hajui kusoma, kuandika na kuhesabu na atalazimika kurudia darasa mpaka afahamu.

Awali, mbali ya masomo hayo matatu, walikuwa wanasoma pia Kiingereza, Sayansi, Haiba na Michezo na Stadi za Kazi. “Sera mpya ya elimu ni bora lakini unashangaa leo mtu anasimama na kuikosoa.

Mtu wa aina hiyo ni wa kusamehewa tu. “Tumeamua kuwapunguzia mzigo wa masomo wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili ambapo sasa watasoma masomo matatu ili kuimarisha uelewa wao na kuzingatia masomo na kama kuna kitu kitakachoongezwa bali ni elimu ya afya tu,” alisema.

Alifafanua kwamba programu ya stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu inalenga katika kuboresha elimu kwa watoto wote wenye umri kati ya miaka mitano hadi 13 nchini katika ngazi za elimu ya awali na msingi, elimu nje ya mfumo rasmi kwa watoto walio katika mazingira hatarishi na elimu ya malezi (Chekechea) kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi.

Naibu Waziri alisema programu hiyo imelenga katika maeneo matano ikiwemo kuwawezesha watoto wa shule za awali na msingi kusoma, kuandika na kuhesabu.

Pia kuwawezesha watoto ambao hawapo katika mfumo rasmi wa elimu katika masomo ya awali na msingi kuweza kusoma, kuandika na kuhesabu, kuongeza uelewa wa watoto wadogo ili kuwawezesha kuingia madarasa ya awali mapema.

Alisema malengo mengine ni kuimarisha mfumo wa elimu na watendaji wake katika maeneo ya mipango, uratibu na uongozi kwa lengo la kuwezesha utoaji wa elimu bora pamoja na kuongeza ushiriki wa jamii katika kuwezesha ujifunzaji wa watoto na ufundishaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.

Walimu wazamia semina Wakati huohuo, takribani walimu 1,000 wanaodaiwa kuzamia semina ya mtaala mpya inayoendelea mjini hapa, wametakiwa kuondoka kwa kuwa hawana mialiko maalumu. Naibu Waziri Majaliwa akizungumza na walimu hao juzi wakati wa kufungua mafunzo hayo, alisema kama kuna mwalimu anajijua amefika kwenye semina hiyo bila kufuata utaratibu ni bora ajiondoe mwenyewe, si kusubiri mpaka aondolewe.

Alisema idadi ya walimu walioalikwa kwenye semina hiyo, imezidi na hiyo inafanya washindwe kupatiwa mahitaji muhimu kama malazi na chakula.

“Nasikia kuna walimu wamekuja kuwakilisha walimu wengine, waliona tabu kupeleka barua kwenye shule husika na kuamua kuteua watu wao kuja hapa,” alisema na kuongeza, “Hapa tulihitaji walimu ambao wanafundisha darasa la kwanza na la pili tu, lakini kama umekuja ukiwa hufundishi masomo hayo ukitoka kwenye mafunzo haya lazima ukafundishe masomo hayo,” alisema.

Pia, alisema inawezekana kuna walimu wakuu wamekuja kwenye mafunzo hayo na kuacha wahusika ambao ni walengwa wakubwa wa mpango huo. Kaimu Katibu Mkuu Tamisemi, Mohamed Pawaga alisema mafunzo hayo yalilenga washiriki 4,430, lakini washiriki waliofika zaidi ya 5,000.

Alisema hali hiyo imeleta mkanganyiko mkubwa katika kuwahudumia, lakini kinachofanyika ni kuhakiki taarifa zao ili wale wanaostahili wabaki na wale wasiostahili kushiriki mafunzo hayo, warudi kwenye vituo vyao vya kazi.

Walimu wanaoshiriki mafunzo hayo ya awamu ya kwanza wanatoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Tanga, Singida, Rukwa, Ruvuma, Morogoro na Pwani . Jumla ya walimu 18,000 wanatarajiwa kupatiwa mafunzo hayo, yatakayotolewa kwa awamu.

Chanzo: Habari leo

0 comments