Thursday 2 July 2015

MAKAMBA: HAKUNA MTIA NIA ANAYEWEZA KUIMEGA CCM

By    
Akizungumza na wanachama wa CCM waliojitokeza kumdhamini katika ofisi ya CCM mkoa Kigoma, Makamba alisema kuwa wale wote wanaotia nia kugombea Urais wa Tanzania lazima wawe na uhakika wa kuweza kumudu majukumu ya kuwatumikia watanzania kwa hali yoyote badala ya kuingia na kufanya majaribio.

Makamba, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, alisema pamoja na nafasi hiyo kutokuwa ya kufanyia majaribio, lakini amesema hakuna mtia nia yeyote anayeweza kuipasua CCM vipande vipande iwapo hatateuliwa na chama hicho kugombea nafasi hiyo.

“CCM ni imara na siku zote itaendelea kuwa imara, wanachama msitishwe na maneno ya baadhi ya watia nia na wapambe wao wanaotangaza kuwa chama hicho kitasambaratika iwapo mgombea wanayetaka apitishwe kugombea Urais jina lake litakatwa, hicho kitu hakitatokea,” alisema mgombea huyo.

Makamba alisema kuwa CCM ni chama kikubwa na hakiendeshwi na mtu mmoja na kwamba katika mchakato huu chama hicho kitachagua kiongozi wake kwa misingi ya kujiamini kwa kuangalia uadilifu wake, utendaji wake na historia yake ndani ya chama.

Akijinadi kwa wanachama wa CCM waliofika kumsikiliza baada ya kudhaminiwa, Makamba alisema kuwa hakuna wakati wa kusubiri kama baadhi ya watu wanavyosema kutokana na umri wake, jambo ambalo amesema kuwa hekima za uongozi hazina uhusiano na umri na kwamba anatosha kuteuliwa kwa nafasi hiyo.


Chanzo: Habari leo

0 comments