Tuesday, 25 August 2015

BILIONI 4.1 ZATOKANA NA FAINI ZA BARABARANI DAR

By    
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekusanya kiasi cha Sh4.1 bilioni kutokana na faini za makosa mbalimbali barabarani.

Katibu wa Kamati ya Usalama Barabarani Kanda ya Dar es Salaam, Peter Sima alisema fedha hizo zilikusanywa kati ya Januari hadi Juni.

Sima alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani katika kanda hiyo.

Alisema mwaka 2014, Sh5.1 bilioni zilikusanywa na kikosi cha usalama barabarani kama faini ya makosa ya usalama barabarani.

Alisema katika kupambana na ajali za barabarani, kamati hiyo itaweka alama za kuvuka kwa miguu katika shule zote za Mkoa wa Dar es Salaam.

“Tunataka wanafunzi wavuke kwa usalama kwenye barabara zetu, tutaweka alama za kuvuka na kuwasimamia madereva wazembe,” alisema.

Akifungua wiki hiyo Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema watu 2,312 wamekufa na wengine 30,314 kujeruhiwa kwa ajali katika kipindi cha mwaka 2011 hadi Juni. Kamanda Kova alisema kati ya hao, madereva wa pikipiki na abiria wao 667 walipoteza maisha.

Alisema katika kipindi hicho, watembea kwa miguu 964 walifariki huku abiria 664 wa mabasi na magari madogo nao wakipoteza maisha. Pia, waendesha mikokoteni 13 walikufa. Kova alisema madereva bodaboda ndilo kundi hatarishi katika ajali za barabarani na hivi sasa wamejaa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)... “Hawafuati sheria na wakisimamishwa na askari wa usalama barabarani hawasimami.”

Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda, Kanda ya Tabata wilayani Ilala, Ramia Mazwela alisema wamekuwa wakipata elimu ya usalama barabarani ili kujikinga na ajali.

Alisema kila dereva wa bodaboda alipewa kikoti maalumu kinachong’aa ili aonekane kwa urahisi barabarani hasa usiku.

“Tunafanya kazi kwa kujiamini sasa kila dereva wa bodaboda ana namba maalumu kwenye ‘jacket’ lake inayomtambulisha kuwa yeye ni nani, hii ni muhimu hata kwa usalama wa abiria,” alisema.

0 comments