Tuesday 25 August 2015

KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI WATOA VIFAA VIPYA VYA KUPIMA MWENDO KASI

By    
Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii 

KIKOSI cha Usalama barabarani  kimetoa vifaa vipya  vya kisasa vya kupima mwendo wa magari.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika vyombo vya habari leo na Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Uslama Barabarani,Mohamed Mpinga,anadai vifaa  vinauwezo wa kurekodi mwendo wa gari na wakati huo huo kuchukua picha ya mnato au video ya gari husika.

Aidha taarifa hiyo ilidai  kuwa ili  kuongeza ufanisi wa vifaa hivi wameelekeza askari wanaoshika vifaa hivyo wasivae sare ili wakishapata mwendo na picha za magari yaliyokiuka mwendo watoe taarifa kwa wenzao wenye sare wafanye ukamataji.

Kamanda mpinga katika taarifa yake kuwa  utaratibu huo unasaidia kuondoa dhana ya askari kujificha na kusimamisha magari kwa kushtukiza na kwa upande mwingine itapunguza tabia ya madereva kupeana ishara kuonyesha mahali walipo askari.

Jeshi la Polisi linawakumbusha Madereva na watumiaji wote wa barabara kuziheshimu sheria na kanuni za usalama barabarani. Aidha nachukua nafasi hii kuwakumbusha askari wote kusimamia sheria na kanuni za usalama barabarani bila woga au upendeleo kwa kuzingatia maadili mema ya kazi.

Hata hivyo  taarifa  hiyo  inawajulisha  watumiaji wote wa barabara hususani madereva kuwa askari wataendelea kuwa wakali sana katika kipindi hiki kwa kusimamia sheria kikamilifu ambapo hatua kali za kisheria zitachuliwa kwa yeyote atakayekamatwa akivunja sheria za usalama barabarani.

Kamanda Mpinga katika taarifa yake amewaasa wananchi na wadau wa usalama barabarani kwa ujumla, watupe ushirikiano zaidi kwa kutoa taarifa za uhalifu wa usalama barabarani, kufuata sheria, kanuni na maelekezo kwa ajili ya usalama wao watumiapo barabara.

"Kila mmoja atambue haki na wajibu wake awapo barabarani ikiwa ni kuwa na subira na kujali watumiaji wengine wa barabara kwani kila mmoja anayo haki sawa ya kutumia barabara. Watoto wasiachwe kutembea barabarani bila ya uangalizi wa watu wazima"amesema Mpinga .

Chanzo: Michuzi Blog

0 comments