Tuesday 25 August 2015

WAZIRI: USHURU WA MABASI NI NGUMU KUPUNGUZWA

By    
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
WAZIRI wa Fedha, Saada Mkuya Salum amewashauri Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa) kulipa ushuru wa asilimia 25 kwa kila basi jipya linaloingizwa nchini kwa awamu.

Waziri Salum alisema madai ya wamiliki hao kutaka ushuru upunguzwe kutoka asilimia 25 mpaka 10 ya zamani hayawezi kutekelezeka kwani ongezeko hilo linatokana na Sheria ya Fedha ya Mwaka 2015.

“Mie kama Waziri siwezi kubadili sheria hii iliyotungwa na Bunge ila naweza kuwaruhusu kulipa kwa awamu,” alisema Waziri Salum wakati anajibu madai ya Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu kwamba mabasi mapya zaidi ya 100 kutoka China yamekwama bandarini Dar es Salaam tangu Julai kwa sababu ya ongezeko la ushuru.

Alisema ataruhusu Taboa kutoa mabasi yao bandarini baada ya kulipa asilimia 10 ya ushuru wa forodha kwa makubaliano kwamba asilimia 15 inayosalia watalipa kwa awamu. “Walipe asilimia tano kwa awamu tatu basi kwani hiyo ipo ndani ya mamlaka yangu,” alisisitiza Waziri wa Fedha.

Alisisitiza kwamba ushuru wa mabasi mapya umekuwa asilimia 25 kila mwaka isipokuwa mwaka wa fedha uliokwisha Juni mwaka huu, ambao ushuru ulipunguzwa mpaka asilimia 10 kuwapa wafanyabiashara muda wa kuagiza mabasi mapya.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Taboa, Mrutu alisema wanachama wao waliagiza magari hayo miezi minne iliyopita na kwamba bajeti zao zilizotokana na mikopo ya benki zilizingatia ushuru wa asilimia 10. “Sasa Waziri anataka tuwe na deni la benki na TRA ambalo tutalipa ndani ya miezi mitano ijayo, siyo jambo rahisi,” alisisitiza.

Mrutu aliitaka serikali kusikiliza kilio chao na kuwaruhusu kulipa ushuru wa asilimia 10 kwani kuchelewa kufanya hivyo kunaongeza gharama za magari hayo.

“Serikali yetu ni sikivu kwa hiyo tunaomba tena katika jambo hili itusaidie kwani mzigo wa madeni tuliyo nayo ni mkubwa tayari,” Katibu Mkuu huyo wa Taboa alisema huku akiiasa serikali kuzingatia umuhimu wa usafiri bora kwa maendeleo ya nchi.

Chanzo: Habari Leo

0 comments