Sunday 6 September 2015

10,000 HAWATAFANYA MITIHANI

By    
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa
WANAFUNZI zaidi ya 10,000 walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2009 mkoani hapa, hawatafanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za utoro na kurudia madarasa.

Hayo yalibainishwa juzi na Ofisa Elimu mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda katika mahojiano na gazeti hili juu ya maandalizi ya mtihani huo mkoani hapa, ambapo alisema yanaendelea vizuri huku nyaraka mbalimbali za mitihani zikiwa zinaendelea kupokelewa.

Alisema wanafunzi 36,273 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mkoani hapa Septemba 9 na 10, mwaka huu. Idadi hiyo ni kati ya wanafunzi 46,596 walioandikishwa mwaka 2009 kujiunga darasa la kwanza.

Kaponda alisema kati ya wanafunzi hao watakaofanya mtihani, 15,746 ni wavulana na wasichana 20,527 kutoka shule 733. Alifafanua kuwa wanafunzi 35,363 watafanya mtihani wa kawaida kwa lugha ya Kiswahili, 881 ni watahiniwa kwa mitihani ya lugha ya Kiingereza, 25 wasioona ambao watatumia nukta nundu na wanne wana uono hafifu.

Akifafanua kuhusu wanafunzi ambao wameshindwa kufanya mtihani kutokana na utoro, Kaponda alisema wanafunzi wengi wamekuwa wakiacha shule kati ya darasa la kwanza na la tano na chanzo kikiwa ni mwamko mdogo wa elimu.

Alisema wanafunzi hao wamekuwa wakitoka kwenye familia ambazo hazina mwamko wa elimu na hukimbilia kuchunga ng’ombe ama kuwa wafanyakazi wa ndani. “Wengi wamekuwa wakitoroka wakiwa kwenye madarasa ya chini na ndio maana idadi ni kubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi kushindwa kumaliza elimu hiyo ya msingi, licha ya kuitikia wito wa uandikishaji darasa la kwanza na shule za awali, wameanza kuchukua hatua dhidi ya wazazi ambao watachangia watoto wao kuacha shule kwa kuwafikisha mahakamani.

Kwa upande wa kurudia madarasa, Ofisa Elimu huyo alisema hiyo inatokana na wanafunzi kutokujua kusoma na kuandika, hivyo kibali maalumu kimekuwa kikiombwa na hiyo imesaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba huku wakiwa hawajui kusoma na kuandika. Mwaka jana jumla ya wanafunzi 38,064 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mkoani hapa.

Chanzo: Habari Leo

0 comments