Tuesday 6 October 2015

ACT WAZALENDO WAHOFIA USALAMA WA SLAA

By    

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimefuta mikutano yote ambayo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alikuwa aifanye kuanzia kesho kupitia jukwaa la chama hicho.

Sababu kubwa imeelezwa ni hofu juu ya usalama ya Dk Slaa ambaye ameachana na siasa tangu chama chake kilipoamua kupokea wanachama wapya kutoka CCM, wakiongozwa na Edward Lowassa ambaye ndani ya muda mfupi amepewa heshima kubwa na hata kufanywa mgombea urais wa chama hicho, nafasi aliyokuwa anaitaka ndani ya CCM, lakini hakupitishwa na vikao muhimu vya chama hicho tawala hivyo kuamua kuhama.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Samson Mwigamba, Dk Slaa tayari alishakubali kupanda jukwaa moja na chama hicho katika kampeni zinazoendelea kwa lengo la kuendeleza vita dhidi ya ufisadi nchini.

“Tunamshukuru sana Dk Slaa kwa imani aliyo nayo juu ya chama chetu na uamuzi wake wa kuikabidhi rasmi ACT-Wazalendo, mikoba yake ya vita dhidi ya ufisadi nchini,” alisema Mwigamba.

Alisema Dk Slaa anaamini kwamba chama hicho cha ACT ndicho chama pekee chenye uhalali na uwezo wa kupambana na ufisadi baada ya chama chake cha zamani (Chadema) kuitelekeza vita hiyo.

Alisema mwanasiasa huyo ilikuwa ashiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea kupitia jukwaa la ACT na alitakiwa aanze na mkutano wa hadhara Iringa Oktoba 7, mwaka huu na baadaye angeendelea na mikutano mingine katika majimbo mbalimbali na kuhitimisha kampeni hizo katika Viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam.

Chanzo: Habari Leo

0 comments