Wednesday 3 August 2016

MENEJA WA DIAMOND AFIKISHWA MAHAKAMA KUU

By    

MENEJA wa msanii Nasib Abdul ‘Diamond Platnumz’ Hamis Taletale ‘Babu Tale’ amefikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akitokea kituo cha Polisi ambako alilala juzi baada ya Mahakama kutoa amri ya kukamatwa kutokana na kutotii amri iliyomtaka amlipe Shekhe Hashim Mbonde Sh milioni 250.

Babu Tale alifika mahakamani hapo mapema kabla ya kuitwa kwa kesi hiyo iliyoanza saa 10:40 asubuhi, miguuni alikuwa amevalia kandambili huku akisindikizwa na Mkurugenzi wa Mkubwa na Wanawe, Said Fella pamoja na msanii chipukizi wa Bongo fleva kutoka lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Raymond.

Meneja huyo anatakiwa alipe fedha hizo kutokana na kuvunja mkataba kati yake na Shekhe Mbonde, kwa kuuza na kusambaza nakala za mawaidha (DVDs) bila ridhaa ya Shekhe huyo, jambo ambalo ni kinyume na haki miliki.

Wakili wa upande wa mdai, Mwesiga Muhingo alidai mahakamani jana mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu, Projest Kahyoza kuwa kesi imekuja kwa ajili ya kusikilizwa ili Babu Tale aieleze mahakama ni kwa nini asifungwe kwa kushindwa kutekeleza hukumu ya Mahakama.

Pia alidai kuwa mdaiwa anatakiwa kueleza mwenzake ambaye ni Idd Tale yupo wapi ili naye aweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani hapo. Wakili wa mdaiwa, Said Elimaamuli aliomba muda kwa ajili ya kusoma nyaraka zinazohusu kesi hiyo kwa kuwa maombi ya utekelezaji wa hukumu ameyapata jana.

Hata hivyo alidai kuwa hapakuwa na amri ya kumkamata na kuletwa mahakamani na kwamba hawajaambiwa kama mdaiwa anatakiwa alipe. Kwa upande wa Wakili wa mdaiwa aliyejitambulisha kwa jina la Mgaya, alidai kuwa wanawasilisha pingamizi la awali kuhusu maombi ya kukamatwa kwa Babu Tale kwamba utaratibu haujafuatwa hivyo aliomba tarehe kwa ajili ya kusikiliza pingamizi hilo.

Pia Elimaamuli aliiambia mahakama hiyo kuwa Babu Tale na Idd Tale wanaishi nyumba moja kama familia hivyo ni kwa nini akamatwe mmoja na kuachwa Idd.

Akijibu hoja za mawakili wa upande wa mdaiwa, Muhingo alidai kuwa maombi ya utekelezaji wa hukumu walipeleka hati ya wito kwa wakili aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, Mgaya Julai 8, mwaka huu ambapo amri ilitolewa na hati ilipelekwa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala.

Muhingo alidai Julai 19 kesi ilikuja tena na Mahakama ilitoa tena amri ya kukamatwa kwa Babu Tale na hati ilipelekwa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni baada ya kupata taarifa kuwa mdaiwa amehamia Kinondoni kutoka Ilala alipokuwa anaishi.

“Taratibu za kukamatwa kwa Babu Tale zimefuatwa na kutokana na yeye mwenyewe kuwepo leo (jana) aeleze kama anaweza kulipa fedha hizo au afungwe gerezani wakati taratibu za kumkamata Idd zikiendelea,’’ alidai Mwesiga.

Licha ya kujibiwa kwa hoja hizo, Elimaamuli alidai kuwa kutofika mahakamani kwa mdaiwa sio tatizo kwa kuwa wakili wao aliwawakilisha hata hivyo alisisitiza kupewa muda kwa ajili ya kupitia nyaraka za hukumu ya Jaji Augustine Shangwa ambayo pia wanaweza kukata rufaa au kuleta mapingamizi.

Wakili Mgaya alidai kuwa Julai 19 mwaka huu, alikuwepo mahakamani na kesi ilikuwa kwa Kaimu Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Juma Hassan ambaye alitakiwa kuahirisha na upande wa mdai ukaleta maombi ya amri ya kukamatwa kwa wadaiwa lakini iliahirishwa.

Msajili wa Mahakama Kuu, Kahyoza alisema kuwa kumbukumbu za mahakama ziko wazi kwamba ilitolewa amri ya kukamatwa kwa mdaiwa kwa Kamanda wa Polisi Kinondoni.

Hata hivyo, aliahirisha kesi hiyo hadi keshokutwa kwa ajili ya kutoa uamuzi na kuamuru mdaiwa (Babu Tale) awe huru kwa sharti la kufika mahakamani hapo siku hiyo.

Februari 18 mwaka huu, Jaji Augustine Shangwa, aliwaamuru wadaiwa kulipa Sh milioni 200 kama fidia ya kuvunja haki miliki ya Shekhe Mbonde na Sh milioni 50 kama fidia ya hasara aliyoipata kutokana na kuvunja makubaliano.

Katika uamuzi wake Jaji Shangwa alisema, Juni 16, 2013, Mbonde aliingia makubaliano na wadaiwa hao na wenzake ya kufanya biashara ya kurekodi mawaidha na kutengeneza nakala DVDs kwa ajili ya kuziuza nchini.

Wadaiwa hao waliahidi kumjengea nyumba, kumnunulia gari na kuitangaza kazi yake pia walimpa Sh milioni mbili na kumnunulia kanzu na kofia (baraghashia) na kurekodi DVDs zenye ujumbe wa Uzito wa Kifo, Fitina Juu ya Wanawake, Umuhimu wa Swala, Mwanadamu yumo ndani ya hasara na Maadui wa Uislamu.

Alisema makubaliano ya awali yalikuwa kurekodi halafu baadaye wakubaliane kuhusu bei na jinsi ya kuziuza, badala yake waliziuza na kuzisambaza nakala hizo na kujipatia faida bila kumshirikisha Mbonde ambaye alitumia ujuzi wake.

Mbonde kupitia Wakili wake Muhingo, Gwamaka Mwaikugile na Clement Kihoko, alifungua kesi ya madai namba 185/2013 akiiomba Mahakama iamuru wadaiwa wamlipe Sh milioni 700, kama fidia ya kuvunja makubaliano na Sh milioni 50 kama fidia ya hasara aliyoipata kutokana na kuvunjwa kwa makubaliano.

Chanzo: Habarileo

0 comments