Sunday, 22 January 2017

MATUMIZI YA BIOTEKNOLOJIA YA KISASA KATIKA KILIMO NI UKOMBOZI KWA WAKULIMA NA TAIFA KWA UJUMLA

 Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (OFAM), Dk. Nicholaus Nyange (kulia), akitoa mada ya matumizi ya Bioteknolojia ya kisasa katika sekta ya kilimo mbele ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba mjini Dodoma.
 Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk.Hassan Mshinda (kulia), akitoa maelezo mbele ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba (wa pili kushoto), alipotembelea shamba la jaribio la mahindi yaliyoboreshwa kwa kutumia Teknolojia ya uhandisi jeni (GMO) lililo chini ya mradi wa Wema katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Makutupora mjini Dodoma juzi. 
 Msafara ukielekea kwenye shamba hilo la majaribio.
 Waziri Tizeba (wa sita kutoka kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na watafiti wa kilimo mbele ya shamba hilo la majaribio ya mbegu za mahindi katika kituo cha kilimo cha Makutupora mkoani Dodoma.
Watafiti na Waziri Tizeba wakijadiliana mbele ya shamba hilo.

Na Dotto Mwaibale, Dodoma

MATUMIZI ya Bioteknolojia ya Kisasa katika Sekta ya Kilimo nchini yataleta mafanikio makubwa kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

Hayo yalielezwa na Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (OFAM), Dk. Nicholaus Nyange wakati akitoa taarifa kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba alipotembelea shamba la jaribio la mahindi yaliyoboreshwa kwa kutumia Teknolojia ya uhandisi jeni chini ya mradi wa Wema katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Makutupora mjini Dodoma. 

"Matumizi ya Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo Tanzania ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho maeneo mengi ya nchi yanakabiliwa na ukame kutokana na tabia nchi" alisema Dk.Nyange.

Alisema taaluma ya uhandisi jeni inawezesha kuhamisha jeni kutoka kwa kiumbe hai kimoja na kuingiza katika kiumbe hai kingine ili kupata sifa lengwa na kutengeneza bidhaa kwa matumizi mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu usalama wa matumizi ya Bioteknolojia hapa nchini alisema ni vema kuanza mchakato wa kuendeleza mazao yaliyofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki (GMO) ambayo yameleta mafanikio makubwa katika nchi nyingine kwa mfano mahindi yanayostahimili ukame na bungua muhogo unaostahimili ugonjwa wa batobato na michirizi kahawia, migomba yenye ukinzani dhidi ya ugonjwa wa mnyauko na pamba yenye ukinzani kwa wadudu waharibifu.

Dk. Nyange alisema Changamoto kubwa iliyopo katika matumizi ya teknolojia hiyo ni kuongezeka kwa upotoshaji kutoka kwa wanaharakati na wapinzani kutokana na 
ufahamu na uelewa wa watafiti, viongozi, wanasiasa na umma kwa jumla kuhusu masuala ya taaluma hiyo kuwa  bado ni mdogo ukiwemo uwekezaji mdogo katika utafiti na maendeleo.1 comment:

  1. Great work, thank you for sharing the informative post.

    ReplyDelete