Showing posts with label Dini. Show all posts
Showing posts with label Dini. Show all posts

Sunday, 8 October 2017

Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Abubakar Zubeir amewaagiza makatibu wa mabaraza ya BAKWATA katika ngazi ya mikoa kufanya sensa ya kubaini waislamu waliopo katika mikoa yao.

Mufti amesema kupitia sensa hiyo BAKWATA itaweza kupanga vyema mipango yake ya maendeleo pindi idadi halisi ya waislamu itakapojulikana.

Chanzo : ukurasa wafacebook wa ITV

Friday, 15 January 2016


Kanisa la urefu wa mita 16 lililojengwa kwa kutumia vigae vya glasi linalofanana na viatu vyenye visigino virefu vinavyopendwa sana na wanawake limejengwa huko Taiwan kwa lengo la kuwavutia wanawake zaidi.

Likiwa limejengwa kwa kutumia vigae vya glasi takriban 320,kanisa hilo la rangi ya buluu lina upana wa mita 10 na limegharimu takriban dola 686,000.

Picha iliopigwa juu ya kanisa hilo pia imeonyesha ukubwa wa kanisa hilo pamoja na uzuri wa eneo lililojengwa.

Jumba hilo la kuabudu linatarajiwa kufunguliwa tarehe 8 mwezi Februari tayari kwa mwaka mpya wa Uchina.

Kiatu hicho kimetengezwa na maafisa wa baraza la miji kusini magharibi mwa pwani ,katika eneo moja la kitalii lenya umaarufu mkubwa huko Taiwan.

Lakini Pan Tsuei-ping,msimamizi wa ujenzi huo,ameiambia BBC kwamba kanisa hilo halitatumika kwa huduma za ibada za kila siku bali hafla za harusi.

''Katika mipango yetu,tunataka kulifanya eneo hili kuwa la kuvutia kimapenzi,kila msichana angepanda kutafakari atakapokuwa bibi harusi alisema'', Pan aliiambia BBC.

Chanzo: BBC Swahili

Wednesday, 21 October 2015

Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemuhukumu kifungo cha maisha jela Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Athanas Ngomai (30), baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wake mwenye umri wa miaka 15.

Pia, mahakama hiyo imetaka mchungaji huyo amlipe fidia ya Sh2 milioni mlalamikaji ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbondole iliyoko Ukonga. Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Ngomai alianza kumbaka mtoto huyo akiwa na umri wa miaka kumi na moja, wakati huo akisoma darasa la tatu.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Ilala, Saidi Mkasiwa alisema Mahakama imemtia hatiani mchungaji huyo baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watano uliotolewa mahakamani hapo akiwamo daktari.

Alisema kutokana na ushahidi huo, upande wa mashtaka ulithibitisha shitaka hilo pasi kuacha shaka, hivyo anamtia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wake. “Mahakama yangu inakutia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wako, utatumikia kifungo cha maisha jela ili liwe fundisho kwa wazazi wengine wenye tabia mbaya kama yako, pia unatakiwa kumlipa fidia mlalamikaji ya Sh2 milioni,” alisema .

Kabla ya hukumu kutolewa, Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwani alitakiwa kuwa mfano bora kwa jamii.

Hata hivyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea.

Mchungaji huyo aliiomba mahakama itende haki kwani yeye hajui sheria na kosa hilo limetengenezwa halina ukweli wowote.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa mahakamani hapo, mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Januari 21, mwaka 2008 katika eneo la Mbondole, Ukonga wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alianza kumbaka mtoto wake huyo akiwa na miaka kumi na moja.

Chanzo: Mwananchi

Wednesday, 23 September 2015

IMG_0481
Mgeni rasmi Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues (wa pili kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan mara baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nyanza jijini Mwanza kushiriki maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani duniani ambapo kitaifa yamefanyika jijini Mwanza. Kushoto ni Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi na wa pili kulia ni Afisa Mfawidhi Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kanda ya ziwa Mwanza, Bw. Ludovick Ringia.(Picha na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
Na Modewjiblog team
WAKATI viongozi wa dini wametakiwa kuacha kufanya siasa na badala yake wahubiri upendo na si upinde, waandishi wa habari wameelezwa kununuliwa na wanasiasa kulainisha maneno yao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho Siku ya Amani Duniani iliyofanyika Mwanza.
Alisema katika mazungumzo yake hayo kukengeuka kwa wanahabari na viongozi wa dini ambao ni wadau muhimu wa amani hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi ni kasoro inayotakiwa kufutwa mara moja.
Akikazia kwa viongozi wa kidini alisema kwamba amani ya nchi inahitaji kulindwa na wote lakini viongozi wa dini wana wajibu mkubwa katika hilo.
Alisema kutokana na wadhifa wake amekuwa akipata habari nyingi ambazo zinakengeuka na zenye mwelekeo hatarishi na nyingi zinakuwa ni za viongozi wa dini.
“Habari zinapoandikwa Tanzania, inapofika saa saba, saa nane ya usiku, mimi huletewa habari nyingi sana, kuziangalia na miongoni mwa habari tulizozizuia ni mbaya kweli kweli zinatoka kwa baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini.” alisema Karsan
IMG_1136
Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho Siku ya Amani Duniani iliyofanyika kitaifa jijini Mwanza.
“Sasa nawaomba sana kwa unyenyekevu mkubwa kwa viongozi wa dini nchini, nawaomba muhubiri upendo na msihubiri upinde!..” alisisitiza Karsan.
Kiongozi huyo wa UTPC yenye wanachama zaidi ya elfu nne alisema kwamba anashangaa viongozi hao wa dini kugeuka wanasiasa kwani anaamini kwamba Kwa Msajili wa Vyama hakuna chama cha dini kilichosajiliwa.
Alisema pamoja na kwamba hakuna chama cha siasa cha kidini kusajiliwa anashuhudia anashuhudia baadhi ya viongozi wa dini wakihubiri siasa.
Pamoja na kuhimiza viongozi wa dini wasitoke katika mstari wao wa kuhubiri amani, alisema kuna kasoro kubwa miongoni mwa wanahabari kwa kuwa wengi wao tayari wamenunuliwa.
“Wanahabari wengi baadhi yao wameshanunuliwa hasa kwa habari zao wanazoandika nyingi wanawachagulia wananchi kwa habari zao za kununuliwa. Andikeni habari na sio kuandika hatari.” alisema Karsan.
Na kuongeza kuwa: “Magazeti yanapiga kura, radio inapiga kura, Televisheni inapiga kura, tena inapiga kura sasa wakati siku ya kura ni Oktoba 25. Acheni kabisa michezo hiyo kwani tunawaomba muwe waandishi wa habari na sio waandishi wa hatari…Andikeni habari na sio hatari!!” alisisitiza Karsan.
Kwa kuzingatia miiko ya taaluma ya habari nchini, alipigilia msumari kwa wamiliki wa vyombo vya habari, wanasiasa kuacha kuwahonga waandishi hasa kwa kutumia fedha ili kulainisha habari huku wakionekana kuunadi Uhuru wakati mioyoni mwao hawana utu.
“Nawaomba wananchi wa Tanzania, msiwachague viongozi wa nchi hii kupitia magazeti, radio na Televisheni. Puuzeni habari zote nendeni kwenye mkutano wa wanasiasa na msikilize kila mgombea anasema nini na kila chama kinasema nini hao wanaoandika kwenye magazeti yao ni yao wenyewe na mengi hayana ukweli.” Alisema.
IMG_1161
Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan akisisitiza jambo kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani duniani jijini Mwanza.
UTPC ina zaidi ya waandishi wa habari 4600 nchini kote ambapo makao yake makuu yapo Mkoani Mwanza.
Pia aliwawaomba wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuhakikisha wanawalipa mishahara waandishi wao kwani hadi sasa baadhi yao wanahabari wanadai mishahara zaidi ya miezi mitatu.
“Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari, ili waandishi waweze kufanya vizuri, basi walipeni mishahara yao. Wapo ambao hadi leo baadhi yao wanawadai mishahara zaidi ya miezi mitatu” alifafanua Karsan.
Karsan aliwataka wamiliki hao kuacha kusimama majukwaani na kujinadi mambo mazuri wakati wanashindwa hata kuwalipa wafanyakazi wao mishahara mizuri na hapo hapo wanataka waandike habari za haki.
Aidha alikemea tabia ya wamiliki wa vyombo vya habari ya kuwachagulia habari wahariri.
Naye mwakilishi Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafa hiyo aliwataka watanzania katika umoja wao kuhakikisha kwamba amani inaendelea kuwapo nchini ikizingatiwa kwamba taifa hili lilipata uhuru kwa njia ya amani.
Alisema Tanzania tangu zamani imeweka mbele mazungumzo katika kutatua mambo mbalimbali na kusema hatua hiyo ya mazungumzo ni hatua kubwa ya kidekrasia ambayo imefanikisha amani na kusema ni tumaini lake kwamba itaendelea kuwapo.
Naye Naibu kamishina wa Polisi Charles Mkumbo ambaye ni kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza akizungumza katika hafla hiyo aliwataka wananchi kutii sheria bila shuruti na kwamba jeshi la polisi limejipanga kuzuia uhalifu na vitendo vinavyotia hofu kuelekea na siku ya uchaguzi.
Alisema jeshi lake limejipanga vyema pamoja na kutumia weledi na busara kuelekea uchaguzi, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Aliwatahadharisha wananchi umuhimu wa kulinda amani kwani gharama ya kuipoteza na kutaka kuirudisha ni kubwa.
IMG_1421
Pichani ni viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini nchini waliohudhuria maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani Duniani ambayo kitaifa yamefanyika jijini Mwanza.

Monday, 14 September 2015

Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakari Zuberi
LICHA ya ongezeko la vifo vya mahujaji katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia, imeelezwa kuwa, hakuna taarifa za vifo vya Waislamu wa Tanzania waliokwenda kutekeleza Ibada ya Hijja nchini humo.

Hayo yameelezwa na Mufti wa Tanzania, Shekhe Abubakari Zuberi jana katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Alisema hadi sasa bado hawajapata taarifa yoyote kuhusu vifo au kujeruhiwa kwa Watanzania waliokwenda kuhiji Makka.

“Napenda kuwataarifu Watanzania wote kuwa waendelee kuwa wavumilivu na kuwaombea wenzetu walioenda kuhiji huko Makka. Hadi hivi sasa hatujapata taarifa yoyote, lakini tunaendelea na juhudi za kufuatilia kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi,” alisema Mufti.

Aidha, alisema tukio hilo ni la kusikitisha na Waislamu wote wawaombee dua kwa Mwenyezi Mungu waliopoteza maisha ili wapumzike mahala pema peponi na kwa wale waliojeruhiwa wapone mapema.

“Tukio hili lilisababishwa na kuanguka kwa winchi iliyokuwa inatumika kwa ujenzi jirani na Msikiti wa Makka na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 107 huku mamia wengine kujeruhiwa vibaya.

“Natoa wito kwa Waislamu wote nchini na misikiti yote kuwaombea dua wenzetu waliotangulia mbele ya haki ili wapumzike salama, sisi wote ni mali ya Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea,” aliongeza.

Alisema mahujaji wa Tanzania walianza kuwasili katika mji wa Makka kuanzia Septemba 9 mwaka huu na hivyo Bakwata pamoja na serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje wanafuatilia ili kujua hali zao na kadhia iliyotokea huko.

“Watanzania waendelee kuwa watulivu na wastahimilivu wakati tunaendelea kufuatilia hali za wenzetu na pindi tukipata taarifa sahihi basi tutawataarifu kupitia vyombo vya habari,” alisema Sheikh Zuberi.

Naye Ofisa Habari wa Shirikisho la Taasisi za Hija Tanzania, Hamisi Juma Tembo, alikaririwa juzi akiwa Uwanja wa Ndege ambako mahujaji wengine walikuwa wakisafiri akisema kwamba taarifa alizo nazo ni kuwa hakuna hujaji wa Tanzania aliyekufa ama kujeruhiwa katika ajali hiyo.

Hivi karibuni kulitokea mvua kubwa na upepo nchini Saudi Arabia iliyosababisha kuanguka kwa winchi hiyo iliyokuwa inatumika katika ujenzi wa kupanua eneo la Tawaf katika msikiti huo wa Makka kwa mita za mraba 400,000 ili kuweza kuchukua idadi ya waumini milioni 2.2 kwa wakati mmoja.

Kwa sasa eneo hilo lina uwezo wa kuchukua watu milioni 2. Tukio lilitokea ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa ibada ya Hija inayofanyika kila mwaka ambayo kwa Waislamu ni moja ya nguzo muhimu.

Chanzo: habarileo

Friday, 11 September 2015

Sheikh Abubakari Zubeiry
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) leo limemchagua Sheikh Abubakary Zubeiry bin Ally  kuwa Mufti Mkuu wa Tanzania.

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo kwenye Ukumbi wa Africa Dream mjini Dodoma, Tume ya Dini ya Kiislamu imemchagua Sheikh Zubeiry kwa kura 310 za ndiyo baada ya kuingia kwenye uchaguzi huo akiwa mgombea pekee.

Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Alhaji Habib Ndassiwa alisema majina mawili yaliyotoka kwenye Baraza la Ulamaa yalikuwa ni ya Sheikh Ally Muhidini Mkoyogole na Sheikh Zubeiry.

Hata hivyo Sheikh Mkoyogole alijitoa na hivyo kumuacha Sheikh Zebeiry kuwa mgombea pekee.

Mufti Zubeiry aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo ya juu katika dini ya Kiislamu mnamo Juni 22 mwaka huu baada ya kifo cha Mufti Issa Shaaban Simba kilichotokea katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

Alitakiwa kushikilia nafasi hiyo kwa muda wa miezi mitatu (Siku Tisini) hadi Septemba mwaka huu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kujaza nafasi hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz