Wednesday, 1 July 2015

WASTANI WA UFAULU SHULE ZA KATA WAONGEZEKA

By    
WASTANI wa ufaulu kwa shule za sekondari za Serikali za kata umezidi kuimarika na kukaribia shule za Serikali ambazo ni kongwe.

Hayo yalibainishwa katika tathmini ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) iliyofanywa kwenye matokeo ya Kidato cha Nne na cha Pili kwa mwaka 2014.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde ameelezea tathmini hiyo wakati wa uzinduzi wa vitabu vya uchambuzi wa matokeo kwa Kidato cha Pili na Nne sambamba na uzinduzi wa mfumo kompyuta wa upatikanaji wa matokeo ya mitihani kwa njia ya simu kupitia ujumbe mfupi (SMS PORTAL).

Alisema wakati mwaka 2012 wastani wa ufaulu wa shule za kata ulikuwa ni asilimia 35.40, ufaulu katika shule za Serikali kongwe ulikuwa ni asilimia 15.81 na kwa mwaka 2014 ufaulu huo umepanda hadi kufikia asilimia 64.49 kwa shule za Serikali kongwe na asilimia 63.56 za wananchi hiyo kuwa na tofauti ya asilimia 0.93.
Aidha, ufaulu wa shule za umma katika mtihani wa kidato cha nne umepanda kwa asilimia 13.30 kutoka asilimia 50.48 kwa mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 63.78 mwaka 2014 wakati ongezeko la ufualu kwa shule zisizo za serikali ni asilimia 1.21 kwa mwaka 2014.

“ Tathmini ya kina ya matokeo imebaini kuwa ufaulu wa shule za Serikali unazidi kuimarika mwaka hadi mwaka. Hata ufaulu katika shule za Serikali za wananchi dhidi ya shule za Serikali Kongwe unadizi kuimarika, pamoja na mafanikio hayo, jitihada za pamoja zinahitajika katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji,” alisema.

Aidha, Msonde alisema takwimu za ufaulu wa mwaka 2014 kimasomo zinaonesha kuwa ufaulu kwa baadhi ya masomo katika mitihani ya darasa la saba, kidato cha pili na nne siyo wa kuridhisha hivyo kuhitajika juhudi za kuboresha ufundishaji na ujifunzaji utoaji wa elimu nchini.

Kuhusu mfumo wa utoaji matokeo kwa njia ya simu, Msonde alisema Baraza limezindua mfumo huo ili matokeo ya taifa yanapatikana kwa urahisi na kuondoa usumbufu kwa watahiniwa na wadau wa elimu bila kujali mahali walipo.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo wa Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema Serikali ya Awamu ya Nne imepanua elimu ya sekondari kwa kujenga shule za wananchi kwa kila kata ili kuongeza fursa kwa Watanzania kupata elimu hiyo.

Alisema matokeo ya juhudi hizo yameanza kuonekana kwa kuwa na ongezeko la wanafunzi wanaohitimu masomo ya kidato cha nne na sita ambapo kutoka mwaka 2015 idadi ya wahitimu ilikuwa ni 87,560 ukilinganisha na wahitimu 244,902 kwa mwaka 2014 kwa kidato cha nne na sita wamepanda kutoka 17,1123 hadi 35,650.

“ Kwa kipindi cha miaka 10 mafanikio ni makubwa, wahitimu wa kidato cha nne wa waliokuwa wanazalishwa kwa miaka mitatu mwaka 2005, lakini mwaka 2014 wanazalishwa kwa mwaka mmoja. Aliongeza: “ Pia shule ambazo baadhi ya watu walikuwa wanazibeza, wakati umefika sasa ambapo hatutazibeza. Watanzania wanatakiwa kuacha kuishi katika historia.”

Kuhusu vitabu vya uchambuzi wa matokeo, Kawambwa aliwataka wadau kuhakikisha wanafikisha vitabu hiyo kwa walengwa kwa wakati ili wavitumie katika kuboresha elimu.

Aidha, Kawambwa amelipongeza Baraza kwa kusimamia ratiba za mitihani na kudhibiti ufujaji wa mitihani kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi (Elimu, Majaliwa Kassimu Majaliwa, amewataka maofisa elimu wa halmashauri zote nchini wa idara ya msingi na sekondari (ambao wote walikuwepo kwenye uzinduzi) kuhakikisha wanavisambaza vitabu kwenye shule zote ndani ya siku 14 ili kuhakikisha vinawafikia wadau wa watumie kujisahihisha kabla ya kufanyika kwa mtihani wa kidato cha nne mwezi Novemba mwaka huu.

“ Nisingependa kusikia kuna Halmashauri imewataka wakuu wa shule waje kuvifuata katika halmashauri, nasisitiza tuvisambaze wenyewe kila shule, maofisa elimu wa mikoa na wakaguzi wa kanda mna jukumu la kufuatilia ili kuhakikisha vimewafikia walengwa na vinatumika kama ilivyokusudiwa,” alisema.

Aidha, Majaliwa amezitaka halmashauri nchini kutumia uchambuzi huo katika kupanga namna ya kuondoa mapungufu yaliyobainishwa katika shule za maeneo yao.


Chanzo: Habari leo

0 comments