SERIKALI imefuta rasmi mafunzo ya ualimu
ngazi ya Cheti yaliyokuwa yakitolewa katika Vyuo vya Ualimu Daraja la A
vilivyopo sehemu mbalimbali nchini. Kufuatia kufutwa kwa mafunzo ya
cheti, watakaochukuliwa kwa ajili ya masomo ya ualimu kwenye vyuo vya
ualimu wa diploma ni waliopata daraja la tatu na kuendelea na
watakapohitimu mafunzo ya miaka miwili ya Diploma (Stashahada) ya ualimu
watapangiwa kufundisha kuanzia shule za awali za serikali, msingi na
sekondari.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk
Shukuru Kawambwa, alisema hayo juzi wakati akizungumza kwa nyakati
tofauti na wanajumuiya ya walimu na wanafunzi wa vipaji maalumu wa Shule
ya Sekondari Kilakala, Mzumbe pamoja na Wanachuo wa Chuo cha Ualimu
Morogoro.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, katika
utekelezaji wa mpango mkakati wa kuboresha sekta ya elimu nchini ,
Serikali imeamua kufuta mafunzo hayo ya ualimu ngazi ya Cheti tangu
mwaka huu na kuweka ngazi ya Diploma.
“Kuanzia mwaka huu tumefuta mafunzo
kutoa cheti cha ualimu...na tumeweka vigezo vipya vya kujiunga na masomo
ya ualimu kwa vyuo vyote vya Serikali na watu binafsi, ni mwanafunzi
aliyepata daraja la tatu na kuendelea “ alisema Waziri huyo na kuongeza
kusema.
“Vyuo binafsi walishachukua wanafunzi wa
ngazi ya Cheti, sasa tumewaambia kuwa mwakani wasiendelee kuwachukua
wafuate utaratibu mpya uliowekwa na Serikali,” alisisitiza waziri huyo.
Hivyo aliwataka wanafunzi wanaosoma
shule za sekondari nchini kuongeza juhudi za masomo ili wapate ufaulu
mzuri utakaowawezesha kuwa na sifa za kujiunga na vyuo vya ualimu ngazi
ya Diploma na kuendelea.
Hata hivyo alisema , mwaka huu wanafunzi
4,000 wa kidato cha nne waliofaulu daraja la tatu na la pili kwenye
masomo ya sayansi, Serikali imewapatia ufadhili wa kuwasomesha Chuo
Kikuu cha Dodoma katika fani ya ualimu wa masomo hayo kwa ajili ya shule
za sekondari na msingi.
Kwa mujibu wa waziri huyo, mbali na
kufuta mafunzo ya ualimu ngazi ya Cheti, Serikali pia imeanzisha mpango
wa kuwaendeleza kimafunzo kazini walimu wa shule za msingi wenye ngazi
ya Cheti ili wafikie ngazi ya Diploma.
Hivyo alisema ,awamu ya kwanza ya mwaka
huu, Serikali imetenga nafasi 935 kwa ajili ya walimu hao wa cheti
waliopo kazini kwa kujiendeleza kwenye Vyuo vya Ualimu vya Diploma ili
waendelee kufanya kazi zao za ufundishaji shule za msingi.
“Lengo ni kuboresha viwango vya elimu
nchini kuanzia shule za awali za Serikali, msingi hadi sekondari,
zifundishwe na walimu wenye Diploma na shahada ya vyuo vikuu.“
Hata hivyo, vyuo vya ualimu vya daraja
la A vitaendelea kuboreshwa kimiundombinu ili kuviwezesha kuchukua
wanafunzi wa masomo ya ualimu ngazi ya Diploma ili kukidhi mahitaji ya
walimu hapa nchini.
Kuhusu shule za vipaji maalumu nchini
zikiwemo za wasichana Kilakala na wavulana Mzumbe, waziri huyo alisema ,
matokeo ya kidato cha nne na sita bado hayaridhishi kulingana na kuitwa
kwao shule za vipaji maalumu.
“Shule hizi za vipaji maalumu
zinakabiliwa na changamoto ya kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani
ya kidato cha nne na sita…shule ya vipaji ni kiongozi wa viwango vya
ufaulu wa hali ya juu ili zioneshe mfano, zinaposhindwa kushika nafasi
za juu hazitoi picha nzuri ya kuitwa hivyo,” alisema Waziri.
Kutokana na kushindwa kufaulisha na
kushika nafazi za juu, waziri huyo aliwataka walimu wote wa shule hizo
kuongeza jitihada katika ufundishaji na pia wanafunzi kusoma kwa bidii
ili matokeo yao yawe bora zaidi kuliko ya shule nyingine za kawaida.
Hata hivyo alisema, Serikali
itayashughulikia matatizo na changamoto mbalimbali zinazokwamisha juhudi
za kufikia mafanikio bora, kwa kutafuta na kuziwezesha kifedha kwa
ajili ya kuboresha miundombinu ya majengo, vitendea kazi vya masomo ya
kujifunzia na kufundishia na usafiri hasa magari.
“Hili la changamoto za shule kongwe za
Serikali sasa jicho letu lipo huko kuziwezesha ili ziwe bora zaidi na
moja ni magari na miundombinu mbalimbali ya shule,” alisema Dk Kawambwa.
Katika hatua nyingine, Kaimu Mkuu wa
Chuo cha Ualimu Morogoro, Azaria Ndyumyeko, alisema katika mpango wa
Diploma ya kawaida elimu ya msingi ya mafunzo kazini (ODPE) mwaka
2014/2015, chuo kilipangiwa walimu 386 wa kujiendeleza na walioripoti ni
157.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Chuo hicho,
kati ya walimu walioripoti wa kike ni 58 na wanaume 99, na wasioripoti
ni 229 na wengi wamekabiliwa na changamoto za waajiri wao ambao ni
wakurugenzi wa halmashauri wameshindwa kuwapatia ruhusa.
0 comments