Rufaa ni hatua ya kisheria ambayo hufikiwa na mhusika katika shauri fulani iwapo hakurushishwa na maamuzi. Rufaa sio mpaka uwe umeshindwa kabisa, hapana. Yawezekana ukawa umeshinda kesi lakini hukuridhishwa na kiwango ulichoshinda.Kwa mfano uliomba wavamizi waondoke katika nyumba yako na hapohapo wakulipe fidia. Mahakama ikatoa hukumu kuwa umeshinda wavamizi waondoke katika nyumba yako lakini ikasema wasikulipe fidia. Mazingira kama haya unakuwa umeshinda lakini ukitaka unaweza kukata rufaa kulalamikia kutolipwa fidia. Kwa hoja hii tunaona kuwa kumbe kukata rufaa si lazima uwe umeshindwa badala yake unaweza kuwa umeshinda lakini ukawa hukuridhishwa na vitu fulani katika hukumu ambavyo unaweza kuvikatia rufaa ili navyo uvipate.
1.AINA ZA RUFAA KATIKA MASHAURI YA ARDHI.
Kisheria rufaa hutofautiana kutokana na aina ya mgogoro ulio mbele. Mgogoro wa kimkataba unazo namna zake na masharti yake katika rufaa, halikadhalika migogoro ya kudai fidia, migogoro ya kikazi, migogoro ya kifamilia na talaka, migogoro ya jinai, migogoro ya kibiashara n.k. Hii ina maana hata migogoro ya ardhi nayo inazo namna zake za rufaa. Katika mashauri ya ardhi mara nyingi migogoro huanzia baraza la ardhi la kata huenda mabaraza ya ardhi ya wilaya, mahakama kuu ya ardhi hadi mahakama ya rufaa. Hizi zote ni mamlaka zinazoweza kuamua mashauri ya ardhi. Aidha aina za rufaa huweza kutokana na mpangilio huu kimahakama. Ipo rufaa inayotoka baraza la ardhi la kata kwenda baraza la ardhi la wilaya. Ipo rufaa kutoka baraza la ardhi la wilaya mpaka mahakama kuu ya ardhi. Na ipo itokayo mahakama kuu ya ardhi mpaka mahakama ya rufaa.
2. NAMNA YA K UKATA RUFAA.
( a ) KUTOKA BARAZA LA ARDHI LA KATA KWENDA BARAZA LA ARDHI LA WILAYA.
Shauri lako la ardhi linapoamuliwa katika baraza la ardhi la kata na ikawa hukuridhishwa na maamuzi ya baraza hilo rufaa yako inatakiwa iende baraza la ardhi la wilaya. Hii ni kutokana kifungu cha 19 cha Sheria ya mahakama ya migogoro ya ardhi sura ya 216 . Zingatia sana kuwa rufaa yako lazima iwasilishwe baraza la ardhi la wilaya ndani ya siku 45 tokea siku hukumu iliposomwa. Aidha muda wa siku 45 unaweza kuongezwa ikiwa kuna sababu za msingi zilizomfanya muomba rufaa kuchelewa kuwasilisha rufaa yake kwa muda.
( b ) RUFAA KUTOKA BARAZA LA ARDHI LA WILAYA KWENDA MAHAKAMA KUU YA ARDHI.
Sheria ya mahakama ya migogoro ya ardhi kifungu cha 38( 1 ) inasema kuwa ikiwa mtu hakuridhika na maamuzi ya baraza la ardhi la wilaya basi anaweza kuomba rufaa kwenda Mahakama kuu kitengo cha ardhi. Rufaa hutakiwa kuwa imewasilishwa ndani siku sitini toka siku ya kutolewa kwa hukumu. Aidha lipo jambo la msingi sana la kuzingatia hapa. Ikiwa shauri lilianzia baraza la kata na rufaa yake ikaenda baraza la wilaya na sasa rufaa yake tena inakwenda mahakama kuu basi rufaa hiyo haitakiwi kupelekwa moja kwa moja mahakama kuu ya ardhi. Kitakachofanyika ni kuwa utandaa rufaa yako na utaiwasilisha palepale mahakama ya wilaya iliyotoa hukumu na mahakama ndiyo itakayowajibika kupeleka rufaa yako mahakama kuu.
( c ) RUFAA KUTOKA MAHAKAMA KUU YA ARDHI KWENDA MAHAKAMA YA RUFAA.
Ikiwa shauri linaloombewa rufaa kwenda mahakama ya rufaa lilianzia baraza la ardhi la kata basi kabla kukata rufaa hiyo ni lazima mhusika kupata hati kutoka mahakama kuu itakayoonesha kuwa kuna jambo la kisheria ambalo mahakama ya rufaa inatakiwa kulitolea ufafanuzi. Na ikiwa shauri lilianzia mahakama ya wilaya basi kabla ya kuomba rufaa kwenda Mahakama ya rufaa mhusika lazima apate ruhusa kutoka mahakama kuu. Nyaraka zinazoambatanishwa ni sababu za rufaa nakala tano, kumbumkumbu za rufaa nakala tano, na risiti kuonesha malipo ya ada husika.
Nimalizie kwa kusema kuwa rufaa katika mashauri ya ardhi ni tofauti na rufaa katika mashauri mengine kama tulivyoona.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
0 comments