Thursday, 30 July 2015

MMLIKI WA ST. MATHEW, ST. MARK ADAIWA TALAKA NA MGAWANYO WA MALI

By    
court_gavel
Na Mwandishi Wetu
MDAI katika kesi ya madai ya talaka na mgawanyo wa mali Magreth Mwangu mkazi wa Mkoani Singida dhidi ya Mkurugenzi wa Shule za sekondari za St.Mathew na St Marks Thadei Mtembei amelalamikia kitendo cha Benki ya CRDB kutoa taarifa zake za benki bila idhini yake wala ya mahakama.
Pia ameilalamikia mahakama ya Mwanzo Kizuiani inayosikiliza kesi hiyo kwa kutumia Wakili wa kujitegemea licha ya kuwa mawakili hawaruhusiwi katika mahakama ya Mwanzo.
Kesi hiyo inasikilizwa na hakimu Rajab Tamaambele.
Wakili huyo amekuwa akimwakilisha mdaiwa ambaye amekuwa hafiki mahakamani tangu kesi hiyo ifunguliwe kwa kile kilichoelezwa wamepata kibali kutoka kwa mwanasheria mkuu wa serikali kinachoruhusu kesi hiyo kusikilizwa na wakili bila mdaiwa kuwepo.
Kwa mujibu wa Mwangu tangu kesi hiyo ianze kusikilizwa mahakamani hapo mdaiwa amekuwa hafiki mahakamani na badala yake amekuwa akiwakilishwa na mtoto wake,Peter Mtembei ambaye ni Wakili hali iliyofanya kesi hiyo mpaka inaisha na kufungwa ushahidi mdaiwa akiwa hajasikiliza shahidi hata mmoja.
Hata hivyo Mmiliki huyo wa St, Mathew juzi alifika mahakamani kufuatia amri ya mahakama kufuatia malalamiko ya mdai aliyokuwa akitoa mahakamani kutokana na Mtembei kushindwa kufika kwenye kesi hiyo tangu ilipofunguliwa na iliyomtaka afike mwenyewe mahakamani hapo na endapo asingefika mahakama ingehamia nyumbani kwake.
Akitoa ushahidi wake, Mtembei alisema alifahamiana na Mwangu wakati akiwa na mfanya usafi katika duka lake la dawa.
Alisema hakuwahi kumuoa mama huyo wala kuishi naye licha ya kuzaa naye watoto watatu.
Alisema mama huyo hana hadhi ya kuwa mke wake kwani ameishia darasa la saba elimu ambayo ni ya chini sana.
“Huyu alikuwa ni mfanya usafi tu ni nesi msaidizi kazi yake ilikuwa ni kufanya usafi na hata kufunga vidonda tu” alisema.
Alisema duka hilo la dawa lilifungwa baada ya kuonekana aliyekuwa analihudumia hana elimu.
Mtembei alisema mdai hana uhusiano na mali alizonazo kwani yeye ana mke wake wa ndoa na huyo alikuwa ni mwanamke tu aliyezaa naye.
“Huyu ni mwanamke tu niliyezaa naye hana haki kwenye mali zangu” alisema
Alipohojiwa na mahakama kama alifunga ndoa na mdai alisema kuwa hajawahi kufunga naye ndoa licha ya kutoa mahari ya Ng’ombe watano. “Nilimpelekea baba yake vindama vitano tu kama zawadi” alisema
Alisema hajawahi kufunga ndoa ya kimila na mdai kama inavyodaiwa na mdai hana haki yoyote katika mali zake.
Kwa upande mwingine mdai alihoji sababu za mdaiwa kwenda Benki ya CRDB na kutoa taarifa za fedha za akaunti yake bila kuwa na amri iliyotolewa na mahakama.
“Mdai kwa kutumia nafasi nzuri ya kifedha aliyokuwa nayo ameweza kwenda benki ya CRDB na kupewa taarifa za fedha kwenye akaunti yangu bila ruhusa yangu au ruhusa ya mahakama jambo ambalo limeniathiri kisaikolojia’ alisema
Hata hivyo hakimuTamaambele alisema hafahamu ni wapi mdaiwa alitoa taarifa hiyo lakini mahakama inaipokea kuwa sehemu ya ushahidi.
Kesi hiyo imepangwa kutolewa hukumu Agosti 25, mwaka huu.
Katika kesi hiyo mdai anaiomba mahakama imuamuru mdaiwa kupa takala,kutoa Sh. Milioni 800 na makazi ya kukaa mdai na watoto wake.

0 comments