Showing posts with label NENO. Show all posts
Showing posts with label NENO. Show all posts

Wednesday, 7 March 2018

Na Jumia Tanzania


Kama unamiliki simu inayotumia mfumo wa Android, basi hautakiwi kijisahau hususani juu ya masuala ya usiri wa matumizi yako na usalama. Hususani kama simu yako ya Android haipati maelekezo ya kusasisha mifumo ya kiusalama mara kwa mara kama watumiaji wa iPhone. Kumiliki simu ya Android inamaanisha kwamba unatakiwa kuwa na umakini wa ziada hususani kwenye progaramu unazozipakua mtandaoni, aina ya mafaili ya APK unayoyaweka kwenye simu yako, kuwa mwangalifu na watengeneza programu wanaozitoa bure. 

Kwa kuwa watumiaji wa Android hawapati fursa ya kujulishwa kuhusu kusasisha usalama wa simu zao kwa mwezi au wiki, kuna hatua muhimu za kufuata ili kuifanya simu yako ya Android kuwa imara dhidi ya mashambulizi kutoka nje - programu zinazolenga kudhuru au kuharibu na kudukua mifumo ya simu. Kuna njia kadhaa za kuilinda simu yako ya Android dhidi ya mashambulio hayo ambayo Jumia ikiwa inajiandaa kuwalete ‘Wiki ya Simu’ wateja wake ingependa kukujulisha kama ifuatavyo:


Funga Skrini Yako. Hili linaweza kuonekana ni jambo la kawaida lakini linaweza kuisaidia simu yako dhidi ya kutumiwa bila ya ruhusa yako au kuwa salama wakati haupo karibu nayo. Iwe umetoka mara moja au umeiacha simu yako mezani unapofanyia kazi, kuiwezesha simu yako kujifunga pindi hauna matumizi nayo kama vile kuweka nenosiri, kufunga kwa kutumia mchoro, uso au namba za siri kunakupatia usalama wa taarifa na kumbukumbu zako kwa hali ya juu.

         

Funga Programu na Mafaili Unayoyatumia. Utaratibu unaweza kuuona kama unachosha lakini ipo siku utakuja kuutambua umuhimu wake pindi programu zako zitakopodhuriwa au kuharibiwa na virusi kwenye kompyuta. Kuna programu kadha wa kadha kwenye ‘Play Store’ ambazo zinaweza kukusaidia kufunga programu na mafaili yako moja baada ya nyingine na kuzilinda dhidi ya kuharibiwa, kudukuliwa, kuharibiwa na virusi pamoja na madhara mengine.


Pakua Programu Kutoka ‘Google Play Store’ Pekee. Unapoweka programu kwenye simu yako, kuna mahala oanakuonyesha kuweka chaguo la kuruhusu kuweka programu kutoka kwa wanaprogramu wasioruhusiwa, hakikisha kwamba sehemu hiyo inaonyesha ‘No’ au ‘Off’ inategemea na mfumo wa android yako. Sehemu hii inatakiwa kuonyesha kutoruhusu, hali hiyo itaifanya simu yako kutoweka programu ambazo hazijaidhinishwa kwenye ‘Google Play Store’. Kupakua na kuweka programu ambazo hazijulikani zimetengenezwa nani, kunaweza kuiweka simu yako kwenye hatari kubwa. Ni muhimu sana kupakua programu kupitia ‘Play Store’ pekee!

Sasisha (Update) Programu zako. Kusasisha au kuzifanyia maboresho programu kwenye simu yako kila mapendekezo kutoka kwa wanaprogramu walioziunda ni muhimu sana. Kila maboresho huja kurekebisha kasoro fulani au kukifanya kifaa chako kuwa imara zaidi. Wanaprogramu hugundua kasoro ndogondogo zinazofanya programu zilizopo sasa kutanya kazi kwa ufanisi, baadhi huwa ni za kiusalama, wanazifanyia kazi, wanazirekebisha na kisha kuziruhusu kupatikana kwa watumiaji kupitia kwenye matoleo yenye maboresho mapya. Hivyo, kama una toleo la programu lililopitwa na wakati kwenye simu yako, ni vema ukazifanyia marekebisho ili kupunguza hatari ya simu yako kuwa hatarini kushambuliwa.

Sasisha Android OS. Toleo la hivi karibuni la android ni Android 8 Oreo. Hakuna shaka kwamba kila toleo jipya la mfumo wa ufanyaji kazi wa simu ya Android huja na maboresho zaidi ya usalama. Iwapo bado unatumia mfumo uliopitwa muda wa android os, upo hatarini kushambuliwa, kuharibiwa, kudukuliwa na hatari zingine tofauti kwenye simu yako. Endapo simu yako haikubali toleo jipya la maboresho ya android os, ni wakati wako kuhifadhi taarifa zako kwenye mfumo wa ‘google drive’ na kuanza kupanga namna ya kupata kifaa kipya chenye toleo la hivi karibuni la OS au angalau kinachotumia Android 7 Nougat.     



Tuesday, 6 March 2018

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora amewataka wafanyabiashara nchini kuhamasika kujiunga na mtandao wa mitaji ya ubia ili kuimarisha vitega uchumi vyao na pia kusaidia kuanzisha viwanda hapa nchini.
Profesa Kamuzora alisema hayo wakati akizindua Mtandao wa Mitaji ya Ubia Tanzania – Tanzania Venture Capital Network jijini Dar es salaam jana.
Aidha Katibu Mkuu huyo amesema uzinduzi wa mtandao huo umefanyika wakati mwafaka ambapo serikali ya awamu ya tano ipo katika mikakati ya kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda,
Aliwataka wananchi kuacha uoga katika ushiriki wa kuwawezesha kuwepo kwa mitaji ya kutosha kwa ajili ya uimarishaji wa uwekezaji nchini Tanzania.
Alisema serikali kwa sasa inafanya kila linalowezekana kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji yanakuwa bora, ndio maana wameanzisha mchakato wa kutengeneza sera ya maendeleo ya viwanda hasa katika sekta binafsi.
Alisema ni vyema wenye viwanda na wananchi wengine kushiriki katika mchakato huo ili kufanikisha nia ya kuipeleka Tanzania katika nchi ya viwanda. Alisema kwa kuwa na sera sheria nyingi zitabadilika na hivyo kupunguza urasimu na pia vikwazo vya kuwezesha kazi katika masuala ya viwanda na biashara.
Pia alitaka wamiliki wa Ubia huo kushirikiana na Costech katika kuhakikisha kwamba viwanda vinaanzishwa na kuendelezwa.
Alitaka kuwepo na elimu ya fedha na mitaji ili wananchi waweze kuthubutu na kufanikisha mitaji.
Mapema Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr. Reginald Mengi amewataka wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa uwazi, kwa kuzingatia sheria za nchi, na kuwa tayari kujifunza maarifa mapya kila fursa inapojitokeza.
Akisitikishwa na mahudhurio duni ya wafanyabiashara katika hafla hiyo alisema kutofahamu undani wa soko la mitaji na fursa zake kunatokana na kutokuwa wazi na kufanya biashara kwa kufuata kanuni.
Akizungumzia kuhusu madai ya kuwapo kwa hali kuwa ngumu nchini Dr. Mengi pia amewataka Watanzania kuichukulia hali hiyo kama fursa ya kubuni biashara itakayowawezesha kupata faida kubwa.
Akiutambulisha Mtandao wa Tanzania Venture Capital kwa wadau, Muasisi wake Bw. Salum Awadh amesema Mtandao huo ni fursa kwa wawekezaji nchini kujipatia mitaji ya kuanzisha ama kuendeleza biashara zao kwa ubia kwa masharti rahisi.
Alisema kwamba wakati umefika kwa Tanzania kusonga mbele kutumia fursa zilizopo duniani za mitaji na kusema jirani zetu wa Kenya wamesonga mbele katika hilo.
Alisema kwamba kutokana na kutojua umuhimu na ushiriki katika mitaji yenye ubia, wananchi wengi wanakimbilia katika mabenki ya biashara ambako pia wanapambana na vikwazo vingine.
Alisema kwa kuwa na kampuni ya mitaji inayoweza kutafuta pia mtaji inayomilikiwa na wananchi wenyewe kupitia mitaji yao kutawezesha kuwapo na uimara wa viwanda na kuongeza idadi zake kwa kuwa mfumo wa fedha wa mitaji ni tofauti na kwenda benki.
Tanzania kwa sasa ina zaidi ya mabenki 50 ambayo yanajishughulisha na mambo mbalimbali yanayogusa biashara na hifadhi ya kawiada.
Alisema mazingira ya sasa yanahitaji mfumo mwingine wa ziada kusaidia upatikanaji wa mitaji nje ya mabenki na kuzinduliwa kwa mtandao wa ubia wa mitaji kutasaidia kuziba pengo lililopo.
Kwa sasa Tanzania kwa rekodi zilizopo inapata asilimia 17 ya mitaji ya ubia ya dola bilioni 2.4 iliyopo duniani huku Kenya ikiwa na nfasi nzuri zaidi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya sekta Binafsi nchini-TPSF Bw. Godfrey Simbeye, baadhi ya viongozi wa taasisi za serikali na wafanyabiashara mbalimbali.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr Reginald Mengi (kushoto), Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora (katikati) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Bw. Godfrey Simbeye (kulia) wakiwasili kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya uzinduzi wa Mtandao wa Mitaji ya Ubia Tanzania – Tanzania Venture Capital Network uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Bw. Godfrey Simbeye (kushoto) akifafanua jambo kabla ya kuanza kwa uzinduzi wa Mtandao wa Mitaji ya Ubia Tanzania – Tanzania Venture Capital Network uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Wanaomsikiliza ni Muasisi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital, Bw. Salum Awadh (wa pili kushoto aliyesimama), Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr Reginald Mengi (wa pili kulia) pamoja Mkurugenzi wa Uwekezaji na Maendeleo ya Viwanda –TPSF, Edward Furaha (kulia).
Muasisi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital, Bw. Salum Awadh akitoa maelezo kuhusu Mtandao wa Tanzania Venture Capital kwa mgeni rasmi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora (kushoto) kabla ya kuelekea kwenye hafla ya uzinduzi wa mtandao huo iliyofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Bw. Godfrey Simbeye (wa pili kushoto) pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr Reginald Mengi (kulia).
Muasisi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital, Bw. Salum Awadh akitoa neno la ukaribisho na kutambulisha mtandao huo ambapo amesema ni fursa kwa wawekezaji nchini kujipatia mitaji ya kuanzisha ama kuendeleza biashara zao kwa ubia kwa masharti rahisi wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa mtandao huo ilyofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr Reginald Mengi akitoa neno la ufunguzi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora kutoa hotuba ya uzinduzi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora akitoa hotuba ya uzinduzi rasmi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital ambapo amesema umefanyika wakati mwafaka ambapo serikali ya awamu ya tano ipo katika mikakati ya kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda katika hafla fupi iliyofanyika kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Uwekezaji na Maendeleo ya Viwanda –TPSF, Bw. Edward Furaha na Aliyekuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mh. Abdullah Mwinyi wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Pichani juu na chini ni sehemu ya wageni waalikwa waliohudhuria uzinduzi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Pichani juu na chini ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr. Reginald Mengi akisalimiana na kubadilishana mawazo na wageni waalikwa waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini- TPSF Dr. Reginald Mengi akibadilisha na mawazo na Afisa Mtendaji Mkuu wa DOB Equity, Brigit van Dijk-van de Reijt wakati wa hafla ya uzinduzi wa wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Wengine ni Mgeni rasmi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Faustine Kamuzora (wa tatu kulia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya sekta Binafsi nchini-TPSF Bw. Godfrey Simbeye (kushoto).
Tanzania Venture Capital Network-TVCN katika picha ya pamoja na mdau aliyewezesha kufanyika kwa uzinduzi wa Mtandao wa Tanzania Venture Capital uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Thursday, 22 February 2018


Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Sunshine uliopo Wilayani Chunya wakati wa ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, Jana 21 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza kwa ukali na baadhi ya viongozi wa Mgodi wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Sunshine uliopo Wilayani Chunya wakati wa ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, Jana 21 Februari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza kwa ukali na mmoja wa kiongozi wa Mgodi wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Sunshine uliopo Wilayani Chunya wakati wa ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, Jana 21 Februari 2018.

Na Mathias Canal, Mbeya

Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amekerwa na usiri wa mapato na matumizi ya muwekezaji wa mgodi wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Sunshine uliopo Wilayani Chunya Mkoani Mbeya.

Mhe Biteko ameonyesha masikitiko makubwa wakati akizungumza na uongozi wa mgodi huo mara baada ya uongozi wa mgodi huo kushindwa kumpatia taarifa ya mapato na matumizi wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani humo kukagua shughuli za uchimbaji Madini.

Kumbukumbu hizo zimekosekana kufuatia viongozi wa ngazi ya juu ya mgodi kutokuwepo kwenye kikao hicho pamoja na kukiri kupokea taarifa ya ujio wake kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya.

Alisema kuwa viongozi hao kukosekana pamoja na kuwa na taarifa ya muda mrefu juu ya ziara hiyo ni utovu mkubwa na nidhamu kwa serikali ya awamu tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.

Alisema kuwa pamoja na kutokuwepo kwao lakini taarifa zilitakiwa kuwepo ofisini kwani ni kosa kisheria kukosekana kwa taarifa za mgodi ilihali sheria ya Madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 inaeleza vyema kuwa mmiliki wa leseni ya Madini anatakiwa kutunza kumbukumbu za mapato na matumizi kwa miaka mitano.

"Endapo atashindwa kufanya hivyo serikali itamchukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kifungo cha mwaka mmoja jela ama faini ya shilingi Milioni 50 mpaka milioni 150" Alisema Naibu Waziri huyo

Mhe Biteko akizungumza huku akionyesha kukerwa na baadhi ya viongozi ambao walikuwepo katika eneo la ofisi ya mgodi huo huku wakishindwa kuhudhuria katika kikao hicho cha kazi alisisitiza kuwa muwekezaji wa mgodi huo anapaswa kuzingatia na kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi.

Sambamba na hayo pia Mhe Biteko aliutaka uongozi wa mgodi huo kutoa taarifa sahihi za uwepo wa mashapu katika mgodi waliyokuwa wakichimba au kama mashapu katika mgodi huo yameisha wafuate taratibu za kisheria za ufungaji wa mgodi ikiwemo kuyarudisha mazingira katika halo take ya kawaida.

MWISHO.

Tuesday, 19 July 2016

PRETTY binti mdogo mwenye umri wa kama mwaka mmoja na nusu unapomzungumzisha, kama watoto wengine wenye afya na uhakika wa malezi anatabasamu na kucheka.

Binti huyu mdogo ambaye analelewa na familia iliyomuasili kwa malezi (hajaasiliwa kisheria) ni miongoni mwa watoto kadhaa nchini ambao wanafaidika na mpango mpya wa kusaidia watoto waliokumbwa na ukatili na unyanyasaji.

Pretty (ambaye si jina lake la ukweli-nimempa jina hilo kulinda haki yake) maisha yake mpaka sasa ni kama kitendawili kibaya ambacho ni Mungu tu alitaka kukifumbua.

Nasema ni Mungu tu kwa kuwa Pretty aliokolewa kutoka katika shimo la choo alilotumbukizwa akiwa ndani ya mfuko wa rambo uliofungwa vyema.

Sajini taji (Staff Sergeant) Pundensiana Baitu wa Dawati la jinsia wilaya ya Kipolisi Mbalizi, anasema kwamba Pretty wakati alipoopolewa katika choo cha mtu binafsi alikuwa na hali mbaya sana kiafya na juhudi kubwa sana ilifanywa na hospitali ya Meta kumrejeshea afya yake.

Akisimulia tukio hilo la kuhudhunisha alisema kwamba usiku wa Machi Mosi, mwaka jana alipokea simu iliyomtafadhalisha msaada ili kuokoa maisha ya mtoto aliyetupwa katika choo kinachotumika, katika eneo la Mlimareli huko Mbalizi.
Sajini taji Pundensiana Baitu wa Dawati la jinsia wilaya ya Kipolisi Mbalizi akizungumza na mwandishi wahabari wa Modewjiblog (hayupo pichani) hivi karibuni.(Imeandaliwa na Zainul Mzige wa Modewjiblog)

Alisema wakati anajaribu kuwasiliana na askari kwenda kuona kama wanahitaji msaada wa Kikosi cha zimamoto, akapokea simu nyingine kwamba wananchi wamebomoa choo hicho na kumtoa mtoto huyo ambaye alikuwa amefungwa katika mfuko wa rambo na kwamba alishaanza kuliwa na wadudu wa chooni.

Aidha aliambiwa katika simu kwamba mtoto huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa wiki moja alikuwa bado anapumua hali iliyomfanya aelekeze polisi kuitengeneza PF 3 haraka na kumpeleka mtoto huyo katika hospitali ya Ifisu ambao nao kutokana na kukosa vifaa vya watoto wa aina yake katika hali ile, walimkimbiza hospitali ya Meta.

Anasema yeye alifika asubuhi kuona hali ya mtoto huyo akiambatana na Ofisa Ustawi wa Jamii na hakupendezwa na hali aliyomkuta nayo mtoto.

Anasema kwamba juhudi za upelelezi kujua mama wa mtoto huyo hazikufanikiwa kwani mtoto alitupwa katika choo binafsi karibu na klabu ya pombe. Hata hivyo anasema baada ya kushindwa waliwaambia wananchi wa eneo hilo kumtazama mtu ambaye wanamtilia shaka na kumfikisha kwao kwa mahojiano.

Mpaka wakati wa kuandika makala haya mtu huyo hajapatikana.

Anasema kutokana na mfumo mpya wa familia ya mfano baada ya wao kama polisi kukamilisha kazi ya usalama na kumkabidhi mtoto huyo kwa Ofisa Ustawi wa Jamii, ofisa huyo alimtafuta mtu ambaye yuko tayari kulea mtoto na kumkakabidhi kwao.

Sajini taji huyo anasema kuwa kuna ongezeko la vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto na kwamba jamii inatakiwa kubadilika na kukubali wajibu wake katika kuhakikisha usalama wa mtoto.
Afisa Ustawi wa Jamii Hospitali ya Kanda ya Nyanda za juu Kusini, Gerald Mwaulesi akielezea tukio la mtoto Pretty mbele ya kamera ya Modewjiblog jijini Mbeya hivi karibuni.

Anasema kabla ya kuanzishwa kwa wilaya mpya wakati bado iko Mbeya amekuwa akishuhudia vurugu nyingi kuhusu ukatili kwa watoto na kwamba dawati lake inachofanya ni kutoa ushauri hasa kwa wadada ambao wanatoa mimba na wengine kutupa watoto wanapopatikana.

Alisema ingawa kuna taratibu ndefu za sheria, mfumo mpya uliokubaliwa na serikali wa kupata familia ya mfano ni mfumo bora wenye kuhakikisha malezi mema na kizazi bora kijacho.

Pretty ambaye kwa sasa anaishi na familia ya mfano yenye watoto sita na yeye akiwa wa saba katika kijiji cha Muvwa kilichopo kata ya Mshewe wilayani Mbalizi ana uhakika na malezi kutokana na mfumo huo mpya.

Na Si ajabu akikua hakuna mtu hata yeye mwenyewe atakayejua kwamba aliokolewa kutoka kwenye shimo la choo alikotupwa na mama katili wiki moja baada ya kuzaliwa kwake na kusaidiwa malezi yake na mfumo wa familia ya mfano.
Dk Sipora Harison Kisanga wa UNICEF kanda ya Iringa akifafanua jambo kwa mwandishi wa habari wa Modewjiblog (hayupo pichani)

Dk Sipora Harison Kisanga ambaye anafanyakazi na UNICEF kanda ya Iringa anasema kwamba ulinzi na usalama wa mtoto ni eda ya wananchi wote kwa ujumla, lakini kutokana na dosari zilizopo ndio maana UNICEF na Tanzania zimetia saini makubaliano yanayowezesha maandalizi ya watu wa kuwapokea watoto waliotelekezwa na wale wenye mazingira magumu ili nao waweze kuwa sehemu ya familia zilizobora.

Anasema kuufanya mfumo huo uwe na utekelezaji uliobora waliendesha mafunzo na kutambua watu wanaoweza kukaa na mtoto, na baada ya kuwakagua wapo katika orodha wakisubiri mtoto yeyote atakayepatikana.

Anasema kutokana na maandalizi hayo ndio maana hata walipompata mtoto Pretty walijua kwamba watampelaka Muvwa kwa familia ambayo iko tayari kupokea mtoto wa aina yoyote na wa umri wowote.

Anasema ni lengo la UNICEF kuhakikisha kwamba haki za watoto zinatekelezwa ikiwamo ya ulinzi na usalama dhidi ya vitu na watu wabaya, huduma za afya, huduma za elimu, haki ya kucheza na haki ya kufundishwa yaliyo mema kutoka kwa wakubwa wao.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mbeya, Lilian Kilongumtwa akielezea tukio la mtoto Pretty aliyetupwa kwenye shimo la choo jijini Mbeya kwa mwandishi wa habari wa mtandao wa Modewjiblog.

Anasema Ofisa huyo wa UNICEF kwamba Mradi wa familia ya mfano ulianzia Temeke na sasa upo Mbeya, Mbarali, na Mbalizi kwa lengo lile lile kuwawezesha watoto hawa kuwa na familia na kuwa salama kuliko kuwapeleka katika vituo vya kulelea yatima.

Mama anayemtunza mtoto huyo pamoja na mumewe, Mama Christer Eliston Mwashusa anasema amefurahi sana kupata mtoto huyo kwani alikuwa tayari kumsaidia kutokana na hofu ya Mungu aliyonayo.

Anasema yeye angelifurahi kama mtoto angemuasili kisheria kwani hali ya sasa ya ulezi pekee anaiona kama haimpi nafasi ya kufanyakazi yake vyema ya kumtunza. Anataka awe mali yake moja kwa moja.

Anasema amepata changamoto nyingi tangu alipomkuta mtoto Pretty hospitali ya Meta, changamoto ambazo zilimuumiza kwanza kama mzazi kwa kutambua kwamba mtoto yule hana wazazi na pia kwa kutambua kwamba ametelekezwa kikatili.
Familia Bw. Juma Mbuza (48) na Bi. Christer Mwashusha (43) inayomlea mtoto Pretty wakifurahi jambo na binti yao baada ya mahojiano na mwandishi wa habari wa Modewjiblog (hayupo pichani).

Pia changamoto ambayo alikumbana nayo ni kule kutambua kwamba mtoto yule kwa sababu ya kuwekwa chooni alikuwa na dhiki kubwa ya afya na hivyo kumfanya kuwa dhaifu.

Anasema hata wakati alipoanza kumtunza changamoto za afya yake zilikuwa kubwa na hasa alipoambiwa kwamba ana ugonjwa ambao ameurithi kwa mama yake, ugonjwa ambao ni upungufu wa kinga na kuanza kumlisha dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kuanzia alipokuwa na miezi miwili hadi minne.

Hata hivyo katika mahojiano na Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka hospitali ya kanda ya rufaa Mbeya (Meta) aliyempokea mtoto huyo Gerald Godfrey Mwambesi alisema kwamba Pretty hakuwa na virusi tangu awali walipompima na kusema kwamba hata vipimo vya hospitali nyingine vilivyosema kwamba ana virusi havikuwa sahihi.

Anasema Pretty alipoteza nguvu ya kinga ya mwili kutokana na kukaa chooni kwa muda na hivyo siku zilivyozidi ndivyo alivyokuwa akiongeza kinga.

Anasema baada ya siku tatu ya kukabiliana na vidonda vyake vilivyotokana na kutafunwa na wadudu chooni na baada ya wiki tatu alionekana kuwa nafuu sana na ingawa mlezi alipata changamoto kiukweli mtoto huyo hakuwa na virusi zaidi ya kupoteza kinga za kawaida ambazo zilitakiwa kurudishwa taratibu.
Dada na kaka wa kufikia mtoto Pretty wakifurahi na mdogo wao mara baada ya kutoka shule.

Anasema mtaalamu huyo kwamba waliongea na wataalamu wa watoto kuhusiana na shida hiyo ya hospitali Mbalizi kumuona mtoto na virusi wakati wao walimpima mara mbili bila kuviona na kusema kwamba hali hiyo inatokana na maambukizi yaliyosababishwa na kutupwa ndani ya choo ambayo yalihitaji tiba ya muda mrefu.

Mlezi anasema kwamba baada ya miezi miwili ya kukaa na mtoto huyo kwa uzuri aliona afya yake inadorora kiasi cha kuhitaji msaada wa tiba na kuanza kwenda hospitali kupata msaada.

Anasema hospitali aliyoenda ilisema mtoto ana maambukizi kutoka kwa mama na kushauri tiba hivyo alipelekwa katika kiliniki ya Beira ambako walimpima na kumwanzishia dozi waliyokuja kuikatisha baada ya kumpima tena kutokana na ufuatiliaji wa hospitali ya Meta na kugundua kwamba hana tatizo la maambukizi ya UKIMWI.

Mlezi wa mtoto huyo alishukuru sana watendaji wa taasisi ya Kihumbe ambao walimsaidia fedha za nauli kwenda katika hospitali kutetea afya ya Pretty na kwamba baada ya matumizi ya dawa na dawa lishe mtoto huyo mwezi uliopita (Juni 16,2016) aliambiwa kwamba mtoto wake hana maambukizi tena.

KIHUMBE, ni taasisi inayofundisha wawezeshaji namna ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu hasa familia zao ili waweze kujimudu wenyewe na kuondokana na matatizo hayo.

Baba mlezi katika familia hiyo yenye watu saba akiwamo Pretty, Juma Mbuza amesifu juhudi za mke wake katika kuhakikisha kwamba Pretty anapata mapenzi yote ya kimama na kuendelea kustawi akiwa katika familia hiyo.

Anasema familia yake inawiwa.kulea mtoto huyo kwa kuwa ndiyo ilikuwa nia yao tangu awali na kwamba awali walitaka kuwachukua watoto waliotelekezwa katika kijiji jirani kwenye tarafa yao. Kuendelea kusoma makala hii bofya hapa

Wednesday, 13 July 2016

Kutokana na baadhi ya watoto kuwa na tabia ambazo hazipendezi watu bila ya kufahamu chanzo chake, imeelezwa kuwa ni vyema wazazi wakajenga mazoea ya kuwafahamu watu ambao wanakuwa karibu na watoto wao ili kuchukua hatua mapema.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Shule ya Watoto ya O'Jays Kiddies Zone, Usia Nkhoma Ledama wakati wa mahali ya nne ya shule hiyo ambapo watoto wa ngazi mbalimbali za madarasa walihitimu.

Usia alisema kuwa wazazi wengi wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kujishughulisha na kazi zao bila kuwa na muda wa kukutana na watoto wao na hivyo kuwa ngumu kutambua chanzo cha tabia ambazo zinaibuka kwa watoto wao kutokana na wao kutowafatilia watu ambao wanakuwa karibu na watoto.

"Tunafahamu wazazi wengi mnakuwa busy na kazi zao na hivyo mtoto akitoka shule anakuwa na dada au kuangalia tv lakini akiwa katika michezo na watoto wenzake mnakuwa hamjui ni vitu vya aina gani wanafanya,

"Nadhani ni vyema sasa kuhakikisha mnawafahamu marafiki wa watoto wenu, marafiki zao wa shuleni na marafiki zao wa nyumbani, huwezi kujua wanafanya nini kama huwafahamu tabia watoto wanaocheza nao lakini kama ukiwajua unakuwa unafahamu rafiki anayefaa ni yupi," alisema Usia.

Aidha aliwatoa hofu wazazi kuwa shuleni hapo wanawafundisha watoto tabia njema na wanawafahamu vyema wanafunzi wao hivyo kazi kubakia kwa wazazi kuhakikisha wanakuwa makini na watoto wanapokuwa nyumbani.
Mkurugenzi wa Shule ya Watoto ya O'Jays Kiddies Zone, Usia Nkhoma Ledama (kushoto) akizungumza na mmoja wa wazazi Bw. Ally Msoya alipowasili kwenye mahafali ya nne ya shule hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa Msasani Tower jijini Dar es Salaam.(Picha zote na Modewjiblog)

Kwa upande wa mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Eda Sanga aliwapongeza wanafunzi ambao wamehitimu masomo na wazazi kwa moyo wao wa kujitoa kuwasomesha watoto wao lakini pia kuwataka kuwasimamia vyema watoto wao ili waweze kufika mbali kielimu.

"Elimu ni muhimu sana kwa watoto wenu wanatakiwa kusoma ili kufika mbali kimaisha niwasihi kuwasimia vyema watoto ili wanapokuwa shuleni wafanye vizuri na wanaporudi nyumbani pia wafanye vizuri," alisema Eda.
Watoto ya O'Jays Kiddies Zone wakitoa burudani kwa wazazi kwenye mahafali ya nne ya shule hiyo.
Mhitimu wa darasa la Laurey, Thomas Mboya akiongoza watoto wenzake kwenye burudani maalum wakati wa mahafali ya nne ya shule hiyo.
Mwanafunzi wa Lilies Class, Iptihaj Kinyaga akiongoza darasa la wanafunzi wenzake kutoa burudani kwa wazazi kwenye mahafali hayo.
Wahitimu wa Laurel Class wakitoa burudani ya kuagana na wanafunzi wenzao katika mahafali ya nne ya shule hiyo.
Pichani juu na chini ni sehemu ya wazazi waliohudhuria mahafali hayo.
Bwana na Bibi Lugoe wazazi wa mhitimu Abigail Lugoe wakiwa meza kuu.
Wazazi wa Watoto ya O'Jays Kiddies Zone wakitazama burudani na vipaji mbalimbali vilivyokuzwa shuleni hapo kutoka kwa watoto wao.
Lantana Class wakitoa burudani kwenye mahafali ya kaka na dada zao
Mkurugenzi wa Shule ya Watoto ya O'Jays Kiddies Zone, Usia Nkhoma Ledama akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mama Eda Sanga kutoa risala kwenye mahafali ya nne ya shule hiyo yaliyofanyika jana kwenye ukumbi wa Msasani Towers jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Eda Sanga akitoa nasaha kwa wazazi na walezi waliohudhuria mahafali ya nne ya darasa la Laurel Shule ya Watoto ya O'Jays Kiddies Zone yaliyofanyika katika ukumbi wa Msasani Towers jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya wazazi na walezi wakisikiliza nasaha za mgeni rasmi.
Wazazi maalum wa mtoto Abigail Lugoe, Bwana na Bibi Lugoe wakitoa shuhuda ya malezi bora na elimu aliyoipata mtoto wao ambaye mwakani atajiunga na darasa la kwanza. Kushoto ni Mkurugenzi wa Shule ya Watoto ya O'Jays Kiddies Zone, Usia Nkhoma Ledama.
Wazazi wakiendelea kushuhudia matukio mbalimbali yaliyojiri kwenye mahafali hayo.
Bw. Ally Msoya na familia yake.
Kutoka kushoto ni Victoria Martin, Thuwein Makamba na Husni Seif, LTE Specialist wa Tigo Tanzania katika mahafali shule ya Shule ya Watoto ya O'Jays Kiddies Zone.
Dada Faiza Ally akibadilishana mawazo na mmoja wa wazazi katika mahafali ya shule hiyo.
Mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Eda Sanga akimtunuku cheti, Joylyn Marandu mhitimu wa Laurel Class katika mahafali ya nne ya shule hiyo.
Wahitimu wakiendelea kutunikiwa vyeti.
Mhitimu Patrick Kasanga akipokea cheti chake. (Picha zaidi ingia hapa)